MSD Yaja na Mpango Kabambe Kuhudumia Wateja Wakubwa (Corporate Customers)
Bohari ya Dawa (MSD) imekutana na wateja wake Wakubwa(Corporate Customers) wanaohudumiwa na Kanda ya MSD Dodoma, kujadiliana na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha na kuboresha upatikanaji wa uhakika wa bidhaa za afya kwa ajili ya huduma maalum zinazotolewa na wateja hao.
Akizungumza wakati wa kikao hicho cha siku mbili, kilichofanyika Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya MSD Dodoma, Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma Bi. Mwanashehe Jumaa, amesema kumekuwepo na changamoto ya kuwahudumia wateja Wakubwa wa MSD, kutokana na huduma maalum wanazotoa, kwani baadhi ya mahitaji yao ya dawa na Vifaa tiba hayako kwenye Katalogia ya bidhaa zinazopatikana MSD, hivyo kupelekea mahitaji hayo kukoseakana ndani ya maghala ya MSD pindi wateja hao, wakiyahitaji.
Bi.Jumaa amesema kutokana na hali hiyo, MSD imekuja na mpango maalum wa kukutana na kujadiliana na Wadau hao, ili kuja na suluhu ya changamoto hiyo, ikiwa ni pamoja na kuainisha mahitaji yao, na kuyawekea mpango maalum wa manunuzi.
Naye Mtaalamu wa Maabara kutoka MSD, Peter Mashosho amesema MSD kwa kutambua umuhimu wa wateja hao kwenye kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, Menejimenti ya MSD imekuja na dawati maalum kwa ajili ya kusimamia na kufuatilia mahitaji ya Wateja hao wakubwa ndani ya MSD, Ili kuhakikisha bidhaa zote ambazo ni non catalogue zinapatikana kwa uhakika, na kwa wakati ili kuwaondolea usumbufu wateja hao.
Kwa upande wake mwakilishi wa wateja hao Bi.Emmiliana Cosmas Bernardo Mfamasia Kiongozi kutoka hospitali ya Benjamin Mkapa, ameupongeza uongozi wa MSD kwa hatua hiyo ya kutafuta Suluhu ya bidhaa hizo, kwani itawaondolea usumbufu wa kutafta bidhaa hizo maalum nje ya MSD, ambapo huchukua muda mrefu na hupatikana kwa bei kubwa.
Aidha, ameongeza kwamba upatikanaji wa uhakika wa bidhaa hizo, utasaidia kuboresha huduma kwa wananchi na kuwaondolea kadhia ya ukosefu huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
- Log in to post comments