MSD na JKCI Kuimarisha Ushirikiano wa Kimkakati Kuboresha Upatikanaji wa Bidhaa za Afya.
#Zanzibar,
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai, amebainisha kwamba Bohari ya Dawa kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wanaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo nchini.
Mavere ameeleza hayo hapo visiwani Zanzibar kwenye Mkutano maalum wa Kimataifa wa Masuala ya Moyo (Cardio Tan 2025) ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kiwete, wakati akiwasilisha mada juu ya changamoto mbalimbali zinazoukabili mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini, hasa kwenye eneo la ununuzi wa bidhaa za programu za moyo.
Mavere amesisitiza kwamba kwa kutumia mfumo wa mpango wa pamoja wa mahitaji (Collaborative Demand Planning), MSD na JKCI wametekeleza ubia wa pamoja (Joint Venture) unaolenga kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa muhimu za huduma za programu za moyo nchini, ili kuboresha afya za wananchi.
“Kwa mara ya kwanza, wataalamu wa moyo wanashirikishwa moja kwa moja kwenye mchakato wa manunuzi, kuhakikisha bidhaa zinazoletwa zinakidhi mahitaji halisi yao ya kitabibu na ushirikiano huu unaonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha huduma za moyo nchini na kuijenga Tanzania yenye afya bora na ustahimilivu”. Alisema Mavere
Ameeleza kwamba kwa kushirikiana na mamlaka za usimamizi wa dawa nchini, MSD na JKCI wanahakikisha bidhaa za afya ya moyo, zinasajiliwa ipasavyo au zinapata kibali maalum cha muda kwa ajili ya manunuzi (One-time Permission), kwani moja ya changamoto ya upatikanaji wa bidhaa nyingi za programu ya moyo, ni kutokana na kutosajiliwa nchini na bidhaa hizo kutokuwepo kwenye katalogia na miongozo ya matibabu ya nchi (Special and Generic Brands).
Katika kuhakikisha bidhaa hizi zenye ubora na viwango vya kimataifa zinapatikana nchini, Mavere amebainisha kwamba MSD inafikiria kushirikiana na makampuni makubwa ya kimataifa kutengeneza bidhaa hizi kwa kandarasi kupitia makampuni ya ndani kwa kufuata miongozo ya WHO ili kuthibitisha bidhaa na wasambazaji.
Katika hatua nyingine Mavere amesisitiza kwamba kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja kwa nchi wanachama wa nchi za SADC, (SADC Pooled Procurement), utawezesha nchi wanachama kupata bidhaa kwa viwango vya chini vya oda (MOQ) kwa ufanisi zaidi, huku bidhaa zinazopendekezwa zikitazamiwa kununuliwa kupitia mikataba ya muda mrefu (Framework Agreements).
- Log in to post comments