Waziri Jenista Mhagama Apongeza Mradi wa Ujenzi wa Ghala la Kisasa la MSD-Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama February 6, 2025 ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ghala la kisasa la kuhifadhia bidhaa za afya linalojengwa na na Bohari ya Dawa (MSD) katika eneo la Kizota, Mkoani Dodoma, na kupongeza hatua za maendeleo ya mradi huo wa kimkakati ambao umefikia. asilimia 85%.
Waziri Mhagama amebainisha kuwa serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya Afya, na imeendelea kujikita kwenye nguzo zinazotuongoza za kimfumo, zinazowezesha upatikanaji wa huduma bora kwenye sekta ya Afya.
"Kazi zilizofanywa zinaonekana, na hata leo tumeona uwekezaji mkubwa wa ghala la hili kubwa na la Kisasa ambalo lina Ubora wa kimataifa, serikali imewekeza hapa zaidi ya Bilioni 23.7 kujenga ghala hili lenye mita za mraba 7,200. Alisema Mhagama
Mhe. Mhagama ameongeza kuwa ujenzi huo pia umeendelea kwenye Kanda ya MSD Mtwara, ambapo zaidi ya Bilioni 18 zimetumika kukamilisha ujenzi, huku akibainisha kwamba ujenzi huo pia utaendelea katika maeneo mengine ambayo ni Mwanza, Chato, Iringa, Moshi, Arusha na Songea.
"Lengo kubwa la jitihada hizi ni kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana kwa wakati na kwa Ubora unaotakiwa, na zinahifadhiwa katika mazingira yanayotakiwa, hivyo Bodi, menejimenti na Serikali ya Dkt. Samia mmeupiga mwingi. Alisisitiza Mhe. Mhagama.
Katika hatua nyingine Mhe. Mhagama ameupongeza uongozi wa MSD kwa kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, ambapo amebainisha kwamba hivi sasa upatikanaji huo umepanda hadi kufikia asilimia 83%.
Ameongeza kuwa MSD ni nyenzo muhimu katika uimarishaji wa huduma za afya katika taifa letu. Hivyo kuipongeza taasisi hiyo kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji endelevu wa bidhaa za afya nchini.
Mhe. Mhagama ameeleza kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na MSD Ili kuhakikisha ndoto na maono haya ya kumkomboa mtanzania, na kuweka usalama kwenye taifa letu yanatimia, kwani afya ya Mtanzania ni usalama wa taifa letu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Bi. Rosemary Silaa ameeleza jinsi MSD ilivyo kwenye mchakato wa kuhakikisha inaongeza hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, ikiwa ni Pamoja na ujenzi wa maghala na ofisi, sambamba na kuboresha mikataba na washitiri na wazalishaji ili kuhakikisha nchi inakuwa salama.
Aidha Bi. Silaa ameendelea kuishukuru wizara ya afya na serikali ya awamu ya sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa usimamizi mzuri na kuendelea kuiwezesha MSD kutekeleza majukumu yake kwa weledi, kwa kuhakikisha fedha za bajeti ya manunuzi ya bidhaa za afya zinapatikana kwa wakati.
Ameongeza kuwa MSD inaendelea na jitihada za kujiendesha kibiashara kwa kuanzisha kampuni Tanzu kwaajili ya kusimamia na kuanzisha viwanda nchini, ili kuwa na upatikanaji endelevu wa bidhaa za afya nchini.
- Log in to post comments