Manunuzi
Bohari ya Dawa (MSD) hununua bidhaa za afya kwa niaba ya vituo vya kutolea huduma za afya vya umma nchini na binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya. MSD pia hununua bidhaa za afya za miradi misonge. Kulingana na uwezo mdogo wa viwanda vya ndani MSD hutegemea asilimia 80 ya dawa kutoka nje ya nchi, asilimia 90 ya vifaa tiba na asimilimia 100 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Manunuzi ya bidhaa za afya, hufuata kanuni na taratibu zilizoainishwa chini ya Sheria ya Manunuzi ya Umma Na. 21 ya mwaka 2004. Mnamo mwaka 2017, MSD ilianza kununua bidhaa za afya moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, badala ya kununua bidhaa hizo kutoka kwa watu wa kati (washiritiri), ili kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, sambamba na kupunguza gharama za bidhaa hizo kwa zaidi ya nusu bei, na robo kwa baadhi ya dawa kutoka bei za awali.
Hata hivyo MSD imeweza kuanzisha viwanda vya kuzalisha dawa zinazohitajika zaidi na inaendelea kushirikiana na sekta binfasi kuanzisha viwanda vya bidhaa za afya kupitia mpango wa mashirikiano baina sekta binafsi na umma, kama ilivyoainishwa kupitia sheria ya Ushirikiano baina Taasisi za Umma na Binafsi ya mwaka 2010 (Public Private Partnership Act, 2010 - PPP). Kutokana na Ushirika huu, MSD inaamini utawezesha Tanzania kujitegemea kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji na upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa hizo muhimu kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wa ubora, Bohari ya Dawa huingiza bidhaa za afya nchini vilivyokaguliwa, kuidhinishwa na kusajiliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA). Usajili wa bidhaa hizo za afya, hufuata hatua za ukaguzi wa ubora, usalama na ufanisi wa matumizi. Hivyo basi, dawa zote mpya zinazoingizwa nchini kutoka kwa wazalishaji au wasambazaji ni sharti zisajiliwe na TMDA, na kupitia mchakato mzima wa uchunguzi wa ubora wa bidhaa za afya huhusisha nyanja zote za ukaguzi ili kujihakikishia ubora, usalama, ufanisi na umadhubuti wa bidhaa hizo katika kipindi cha muda wake maalum ulioainishwa kitaalamu. Aidha vifungashio na uwekaji nembo/alama/lebo au jina la bidhaa ni eneo lingine linalotiliwa mkazo wakati wa ukaguzi.