Viwanda vya MSD
- USULI WA KIHISTORIA
Bohari ya Dawa (MSD) ilitokana na mabadiliko ya iliyokuwa Bohari Kuu ya Dawa (Central Medica Stores). CMS ilikuwa idara chini ya Wizara ya Afya ambayo ilikuwa na jukumu la ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya nchini. Ilifanya kazi chini ya ushawishi wa wizara tatu, yaani Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na Wizara ya Ujenzi.
Mara tu baada ya Uhuru wa Jamhuri ya Tanganyika ya wakati huo mwaka 1961, Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika alifanya ziara katika nchi za Kisoshalisti kama vile China, Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti ya Urusi – USSR, Korea n.k. katika ziara yake hiyo, China ilikubali kuisaidia Tanganyika katika Sekta ya Viwanda ikiwa ni pamoja na Utengenezaji wa Madawa.
Mwaka 1968, kiwanda cha kwanza cha umma cha kutengeneza dawa kilizinduliwa katika eneo la Keko jijini Dar es Salaam. Huu ulikuwa msaada kamili kutoka kwa serikali ya China. Bidhaa zilizotengenezwa zilisambazwa kote nchini kupitia Bohari Kuu ya Dawa (CMS). Kiwanda hicho kikawa sehemu ya CMS chini ya wizara ya afya. Hata hivyo, katika miaka ya 1990, viwanda vingi vilivyomilikiwa na umma vililazimika kufunga milango kutokana na changamoto za kiuchumi ambazo zilisababishwa na uzembe na wafanyakazi wasio na uzoefu wa kusimamia viwanda vya uzalishaji. Masharti yaliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia kama suluhisho la kiuchumi kwa nchi zinazoendelea yalisababisha ubinafsishaji wa viwanda vingi vinavyomilikiwa na umma. Kiwanda cha kutengeneza dawa cha Keko pia kilibinafsishwa.
Kwa upande mwingine, mwaka 1993 CMS ilibadilishwa na kuwa MSD (Medical Stores Department) kupitia Sheria ya Bunge namba 13 ya 1993. MSD ikawa idara inayojitegemea chini ya Wizara ya Afya inayofanya kazi kwa misingi ya kibiashara. Ilipewa mamlaka ya kununua, kuhifadhi na kusambaza bidhaa za afya kwa vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na umma.
- II. WAZO LA KUANZISHA VIWANDA VYA BIDHAA ZA AFYA MSD.
Wazo la kuanza kujihusisha na utengenezaji wa bidhaa za Afya katika MSD liliibuka tena mwaka 2013/2014 ikiwa ni moja ya mikakati ya kuboresha upatikanaji wa shehena ya bidhaa za afya nchini ambayo ilitokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali na utoaji wa fedha kwa MSD. Licha ya juhudi zote hizo, haikuwezekana kuanza utengenezaji kwa sababu hakukuwa na mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.
- III. UPANUZI WA KAZI ZA MSD
Hadi ilipofika mwaka 2021, wazo la MSD kuwa na viwanda ndipo lilipoanza kutumika. Sheria ya MSD namba 13 ya mwaka 1993 ilifanyiwa marekebisho ili kuendana na kazi ya nne ya ‘Uzalishaji’. MSD sasa ina mamlaka ya kisheria ya Kununua, Kuzalisha, Kuhifadhi na Kusambaza bidhaa za Afya nchini.
- IV. . SABABU ZA KUWA NA VIWANDA MSD
Zifuatazo ni sababu zilizoisukuma MSD kujihusisha na viwanda vya utengenezaji wa bidhaa za Afya:
a. Kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kupunguza muda wa manunuzi
Mzunguko mrefu wa manunuzi unaohitajika katika sheria ya manunuzii hufanya iwe vigumu kupata bidhaa za afya kwa wakati inapohitajika. Siku zinazohitajika kuagiza bidhaa hadi afya hadi kufika nchini si chini ya miezi tisa. Kwa utengenezaji wa ndani, dawa zinaweza kupatikana kwa muda mfupi na haraka iwezekanavyo.
b. Kutopoteza fedha za kigeni ambazo ni hupatikana kwa jasho
Ili kuagiza bidhaa yoyote nje ya nchi, fedha za kigeni hutumika. Kwa hivyo uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya utaokoa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni ambazo zinaweza kutumika kwa ajili ya mahitaji mengine muhimu.
c. Kupunguza gharama za uagizaji wa bidhaa nje ya nchi.
Kupunguza gharama za uagizaji wa bidhaa kutoka ng’ambo kunapunguza bei za bidhaa za afya zinazozalishwa hapa nchini zikiwa zenye viwango sawa vya ubora.
d. Kutoa ajira kwa watu wa Tanzania
Utoaji wa ajira kwa Watanzania una faida kubwa zaidi na matokeo ya moja kwa moja kwa ustawi wa watu wa Tanzania.
e. Kulinda Taifa dhidi ya uhaba wa bidhaa za afya.
Usalama wa Kitaifa wa bidhaa za Afya daima huwa hatarini iwapo kuna dharura za kimataifa kama vile magonjwa ya milipuko, k.m. UVIKO -19, nk ambapo ni vigumu sana au haiwezekani kuagiza bidhaa kutoka ng'ambo.
f. Kuzingatia sera ya Taifa ya Viwanda.
Tanzania imeanza kuwekeza kwenye Viwanda vya Uzalishaji ili kupunguza utegemezi kutoka nje ya nchi katika upatikanaji wa bidhaa zinazotumika kwa wingi chini.