Upatikanaji wa Dawa nchini, Wapaa hadi Kufikia 81%
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), Mavere Tukai amesema kuwa upatikanaji wa dawa nchini umefikia asilimia 81 mwezi Juni 2023 kutoka asilimia 57 mwezi Juni 2022 jambo ambalo limechangia kurahisisha utoaji huduma nchini.
Ameyasema hayo Septemba 27, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mavere amesema kuwa upatikanaji wa bidhaa za afya nchini umeendelea kuimarika siku baada ya siku kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Rais Samia umechangia upatikanaji wa bidhaa za afya kutoka asilimia 51 mwezi Juni 2022 hadi kufikia asilimia 64 Juni 2023,” amesema Mavere.
Ameongeza kuwa MSD imekuwa ikishirikiana na sekta binafsi katika kufanikisha usambazaji dawa ambapo ina majukumu manne ikiwemo uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji.
“Uzalishaji unafanyika kupitia viwanda vyetu ikiwemo kiwanda cha Keko ambacho tunakimiliki kwa asilimia 70 na Serikali huku sekta binafsi ikimiliki asilimia 30” amesema.
Amesema, pia wana jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa uhakika katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini na wamekuwa wakitekeleza hilo kwa ufanisi mkubwa.
Mkurugenzi Mkuu huyo amefafanua kuwa, MSD imekuwa ikifanya usambazaji wa bidhaa za afya moja kwa moja kwenye vituo.
“Usambazaji unafanyika kila baada ya miezi miwili tukiwa na magari zaidi ya 185 na makabidhiano yanafanyika kwa mfumo wa PoD (kupitia TEHAMA),” amebainisha.
Amesema, kupitia kanda zake 10 ambazo zinajumuisha mikoa ya Dar es Salaam,Tanga, Kilimanjaro, Iringa, Mbeya, Mwanza, Tabora,Kagera,Mtwara na Dodoma wanahudumia zaidi ya vituo 7,600 vya afya.
Vilevile amesema, fedha iliyopokelewa mwaka wa fedha 2022/23 ni shilingi bilioni 190.3 ikilinganishwa na shilingi bilioni 134.9 mwaka wa fedha 2021/22, sawa na asilimia 95.
- Log in to post comments