UNFPA Yatoa Msaada wa Dawa za Uzazi wa Mpango kwa Serikali ya Tanzania
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu UNFPA limeikabidhi Serikali ya Tanzania msaada wa dawa za uzazi wa mpango.
Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika Bohari ya Dawa (MSD) Mwakilishi wa UNFPA nchini Tanzania Bw. Mark Bryan Schreiner amesema msaada huo ni sehemu ya jitihada za UNFPA kuisaidia Serikali ya Tanzania kuboresha huduma za uzazi wa mpango kwa wananchi.
Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa mshirika mkubwa wa UNFPA, katika utekelezaji na uboreshaji wa huduma za uzazi wa mpango jambo ambalo linachagiza katika stawisha afya za wananchi hasa wa hali ya chini.
Naye mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Felix Bundala ameishukuru UNFPA kwa kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania hasa katika kuisaidia Tanzania kwenye nyanja mbalimbali za uboreshaji wa huduma za afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai amesema MSD imepokea dawa hizo na jukumu la MSD ni kuhakikisha zinafika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini, lengo likiwa kuboresha huduma za afya hasa ya mama na mtoto.
- Log in to post comments