Mkoa wa Dodoma Wajipanga Kuboresha Upatikanaji wa Bidhaa za Afya
Meneja MSD Kanda ya Dodoma Bi. Mwanashehe Jumaa ameuomba uongozi wa Timu ya Usiamizi wa afya Mkoa wa Dodoma (RHMT) kuratibu na kusimamia uwasilishwaji wa maombi ya mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya kwa wakati na ulipaji wa madeni, ili MSD iendelee kutoa huduma kwa ufanisi na kwa wakati.
Bi.Jumaa ametoa rai hiyo mwishoni mwa juma, mbele ya timu hiyo, chini ya uongozi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Thomas Rutachunzibwa, wakati wa kikao cha kujadili namna ya kuboresha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya mkoani humo, kilichokutanisha ujumbe kutoka MSD na uongozi wa afya Mkoani humo.
Bi. Jumaa amebainisha kwamba uwezo wa MSD kuhudumia wateja wake kikamilifu, unategemea mambo mengi ikiwemo rasilimali fedha, hivyo kuviomba vituo vyenye madeni kulipa kwa wakati au kupunguza madeni yao, ili kuipa MSD msuli wa kuendelea kuagiza bidhaa za afya, na kuhakikisha bidhaa zinakuwepo ghalani muda wote.
Pamoja hilo, Bi. Jumaa ameupongeza uongozi wa Afya Mkoani hapo, kwa kuitisha kikao hicho baina ya pande hizo, ambacho amesema kimeleta majadiliano yenye tija, na kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya Mkoani humo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dkt. Rutachunzibwa ameitaka timu hiyo ya RHMT Dodoma, kusimamia watendaji wa Afya Mkoani humo kwa kuhakikisha wanachakata na kuwasilisha mahitaji yao kwa wakati MSD, Ili waweze kuhudumiwa kwa wakati, na huduma za afya ziwe endelevu.
Dkt. Rutachunzibwa ameilekeza Timu hiyo ya RHMT kuhakikisha Watumishi wa Afya, wanatumia weledi wao, kuhakikisha wanachakata mahitaji yao kwa usahihi, ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa bidhaa za afya vituoni, kutokana na maoteo yasoyokidhi mahitaji.
Sambamba na hilo Dkt.Rutachunzibwa ameiagiza timu hiyo ya RHMT Dodoma kama wasimamizi wa vituo vya afya, kuhakikisha mahitaji ya bidhaa za afya Mkoani humo, yanawafika mkoani hapo kabla ya tarehe tano ya Kila mwezi, ili yatathiminiwe na kupitishwa kisha kuwasilishwa MSD kabla ya tarehe ya 10 ya mwezi husika, kama mwongozo wa ILS unavyoekekeza.
Katika hatua nyingine amevielekeza vituo vya kutolea huduma za afya Mkoani humo, kulipa madeni yao MSD, ili kuhakikisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya Mkoani humo haukatiki, bali unakuwa endelevu
Aidha, ameitaka Timu hiyo ya RHMT kwa kushirikiana na MSD kuhakikisha wanavitembelea vituo vyote vyenye madeni MSD na kubaini uhalisia wake na kisha kuhakikisha vinafanya malipo kupitia vyanzo vingine vya mapato.
- Log in to post comments