Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Aipongeza Kanda ya MSD Tanga kwa Kuvuka Malengo ya Mauzo
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD) Dkt. Rukia Mwifunyi amepongeza Kanda ya MSD Tanga kwa kuvuka malengo ya mauzo, katika robo mwaka ya kwanza ya mwaka kwa asilimia 12.
Mjumbe huyo wa Bodi, ambaye ni mlezi wa Kanda ya MSD TANGA amefuatana na Meneja Huduma za Sheria MSD, Elisamehe Macha katika ziara ya kutembelea wateja wanaohudumiwa na Kanda ya Tanga,ziara ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka thelathini (30) ya utendaji wa MSD tangu kuundwa kwake.
Akizungumza na watumishi wa kanda ya Tanga Dkt. Mwifunyi amemwelekeza Meneja wa kanda ya Tanga, Sitti Abdurahman kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu madeni wanayowadai wateja wao.
Naye Meneja wa Kanda hiyo Bi. Sitti Abdulahman amesema Kanda hiyo imejipanga kimkakati kuhakikisha inakidhi matakwa ya wateja wake, kwa kuhakikisha inakuwa na bidhaa za afya wakati wote na kuwahudumia wateja kwa weledi mkubwa.
Aidha, ameongeza kuwa Kanda hiyo pia imejidhatiti katika kuhakikisha inafuatilia madeni yake, na kuhakikisha inapunguza madeni ya wateja wake, ili kuipa MSD msuli wa kuendelea kuagiza bidhaa za afya.
Ziara hiyo inaendelea kwa kutembelea Hospitali ya mkoa Bombo, na kituo cha afya Nkumba kilichopo wilaya ya Muheza, Tanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho maalum ya miaka 30 ya MSD, toka ilipoanzishwa mnamo mwaka 1994.
- Log in to post comments