Dkt. Mollel Aishauri MSD Namna ya Kuboresha Upatikanaji wa Bidhaa za Afya Nchini.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameishauri Bohari ya Dawa (MSD) kutengeneza mpango wa muda mrefu wa kuzungumza na wazalishaji dawa na bidhaa nyingine za afya kutoka nchi zinazozalisha bidhaa hizo, ili kuja kuwekeza nchini Tanzania, hatua ambayo itarahisisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.
Naibu waziri ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Kimataifa ya wadau wa bidhaa za afya ya Afrika Mashariki yaliyoanza leo jijini Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa MSD pia iangalie namna ya kuingia mikataba na nchizinazozalisha bidhaa za afya kurahisisha kununua moja kwa moja kutoka kwao, ili kupunguza gharama na kuwezesha kupata bidhaa za kutosheleza mahitaji.
Kiongozi huyo pia amewahimiza wazalishaji hao wa nje kuja kuwekeza nchini Tanzania kwa kuingia ubia na serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano MSD Bi. Etty Kusiluka, amemshukuru Dkt. Mollel kwa ushauri, na kuahidi kuufikisha kwenye Menejimenti ya MSD ili uweze kufanyiwa kazi.
Aidha, ameendelea kuwakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kutembelea banda la MSD lilipo kwenye maonyesho hayo, ili waweze kupata taarifa mbalimbali zinazohusiana na MSD, sambamba na kufahamu namna taasisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake.
Maonyesho hayo ya Kimataifa ya bidhaa za afya ya Afrika Mashariki yanafanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa Diamond Jubilee, ulioko jijini Dar es Salaam, kwa kuwakutanisha Wadau kutoka nchi mbalimbali.
- Log in to post comments