Changamoto za Usambazaji wa Dawa na Vifaa Tiba- Wilaya ya Ludewa
Changamoto za jiografia zilizopo katika Wilaya ya Ludewa zimekuwa zikisababisha ugumu wa kufikisha dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya pamoja na kusafirisha wagonjwa hasa wanapopata rufaa kutoka vituo vya pembezoni kwenda Hospitali ya Wilaya.
Hali hiyo inatokana na baadhi ya vijiji kuwepo katika miamba na vingine kwenye mwambao wa ziwa nyasa ambako hulazimika kusafiri majini kwa saa tatu mpaka kumi na mbili.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Dk Stanley Mlay alipozungumza na Mwananchi Novemba 19, 2023 akiongeza kuwa asilimia 80 wanaagiza vifaa kutoka Bohari ya Dawa (MSD) na kuhakikisha vinafika kwa walengwa.
“Katika zoezi la kufikisha kumekuwa na changamoto kadha wa kadha tunazokabiliana nazo, ikiwemo baadhi ya vituo vilivyopo mwambao wa ziwa nyasa kutokuwa na miundombinu rafiki kwa maana ya barabara.
“Vituo vipo kwenye miamba kwahiyo kumekuwa na changamoto ya kukosekana kwa barabara rasmi, ambayo inaweza kutumika kwa ajii ya kusafirisha vifaa husika,” amesema.
Amesema muda mwingi hulazimika kusafirisha kwa njia ya maji kutumia boti na baadaye vinashushwa nchi kavu na kunafanya utaratibu wa kutafuta watu wenye nguvu ili kubeba kupanda milima mpaka kuvifikia vijiji.
Dk Mlay amesema Wilaya hiyo wana changamoto zingine kwa baadhi ya vituo ambavyo vipo katika maeneo yanayofikika lakini kutokana na miundombinu kuharibiwa na mvua, imekuwa ngumu magari na pikipiki kupita kwa urahisi.
Amesema hali hiyo huwafanya watumie njia mbadala kuhakikisha dawa zinafika na maeneo mengine yana umbali wa kilomita 4 hadi 10.
Hata hivyo Dk Mlay anasema kutokana na kasi ya ujenzi wa vituo, vipo vinavyojengwa maeneo ambayo hakuna barabara hivyo huangalia namna ya kufikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi na mara nyingi hufikisha kwa miguu au baiskeli.
“Lakini kadri siku zinavyokwenda kuna maboresho ya miundombinu, changamoto zimekuwa zikipungua kwahiyo nasi tunahakikisha vifaa vinafika ili huduma ziendelee kutolewa.
“Kuna baadhi ya maeneo kutokana na kutokuwepo kwa barabara inalazimika mgonjwa abebwe mpaka sehemu ambayo tunapata miundombinu kwa ajili ya kumsafirisha…
“Hata anapobebwa tunahakikisha taratibu zingine zinafanyika ili mgonjwa afike hospitalini na wataalamu wetu wana mafunzo ya kutosha wanaongozana na mgonjwa ili waweze kupambana na dharura ambazo zitajitokeza,” amesema Dk Mlay. Amesema yapo baadhi ya maeneo yenye miundombinu ya maji ambako nako wanahakikisha wanafikisha huduma.
“Kuna vituo visivyopungua 10 ambavyo vinapakana na mwambao wa Ziwa Nyasa na vingine vinapakana Mbinga, huko tunalazimika kusafirisha kwa boti sasa unakuja kukuta vituo hivyo boti tunazotumia katika baadhi ya vituo si chini ya saa tatu mpaka nne kufikisha vifaa hivyo, lakini tunahakikisha tunafikisha.”
Anataja baadhi ya vituo kama zahanati ya Nkwimbili, Masimavalahu, Lupingu, Ntumbati, Ndowa, Lubila, Nkanda na kituo cha afya Makonde zilizopo nchi kavu lakini kutokana na miundombinu wanalazimika kubeba vichwani kwa pikipiki na baiskeli.
Amesema MSD wamekuwa wakijitahidi bidhaa za msingi zinazoagizwa zinapatikana na huomba watumiwe mahitaji mapema ili wapate muda wa kutafuta bidhaa zilizoingizwa ili zipatikane kwa wakati pia hata bei ya bidhaa wanazonunua huko ni ndogo kuliko kwa wazabuni.
“Kwa sasa MSD wamehakikisha wanakuwa na utaratibu wa kufikisha bidhaa moja kwa moja vituoni hapo nyuma, zilifikishwa hapa kituoni na sisi kama Wilaya tulizisambaza vituoni sasa ile ilikuwa na changamoto yake kiusafirishaji,” amesema Mlay.
Licha ya maeneo hayo kutofikika, Serikali imewezesha ujenzi wa barabara ya zege kwenye kipande kinachoingia kijiji cha Lupingu kilichopo ziwani ambacho ndicho kinachotumika kama njia ya majini kuelekea vijijini vingine visivyofikika mwambao wa ziwa hilo.
Wananchi wa maeneo hayo, wamesema wanashindwa kuhama kwa kuwa wamezaliwa huko, licha ya kuwepo kwa zao moja pekee linalostawi ambalo ni muhogo.
"Mababu zetu waliokuja huku, tumezaliwa na kusoma hukuhuku, hatuwezi kuhama. Ijapokuwa maisha ni magumu maeneo haya ila tumezoea kula mihogo na dagaa au samaki ambao tunawavua Ziwa Nyasa," amesema Monica Kiswaga.
Meneja wa MSD Kanda ya Iringa, Robert Lugembe amesema wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuhakikisha bidhaa zote za afya zinawafikia walengwa kwa wakati kwa kadri walivyoomba.
Amesisitiza kwamba licha ya changamoto ya miundombinu bado MSD imekua ikihakikisha inafikia vituo na zahanati zote ambazo ni vigumu kuzifikia.
Ameongeza kwamba MSD itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, hasa upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba.
- Log in to post comments