Skip to main content

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Aipongeza MSD kwa Maboresho ya Huduma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameupongeza uongozi wa Bohari ya Dawa (MSD) kwa mabadiliko makubwa yanayoendelea katika taasisi hiyo, ambayo kwa kiasi kikubwa yamewezesha kupunguza malalamiko ya uhaba wa bidhaa za afya nchini, mathalani malalamiko ya uhaba wa dawa.

Mhe. Senyamule ameeleza kwamba awali wakienda kwenye mikutano ya hadhara kuongea na wananchi, walikumbana na malalamiko mengi ya uhaba wa dawa, lakini hivi karibuni hali imebadilika, japokuwa bado kuna changamoto, lakini angalau inatia moyo kuona kuna mageuzi yanafanyika.

Mhe. Senyamule ametoa pongezi hizo leo wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa wateja na wadau wa MSD Kanda ya Dodoma, ambao ni kutoka mikoa ya Dodoma, Singida na Halmashauri ya Kiteto, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa OSHA jijini Dodoma.

Hata hivyo Mkuu huyo wa mkoa amesisitiza kwamba huwezi kuongelea maendeleo ya sekta ya afya bila kumtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani ameleta mapinduzi makubwa, katika kipindi kifupi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

“Tunapoongelea maboresho ya sekta ya afya na mabadiliko ya huduma hatuwezi kuacha kumtaja Mhe. Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan, kama kiongozi mkuu aliyeongoza mapinduzi haya, kwani tumeshuhudia ongezeko kubwa la bajeti ya bidhaa za afya, miundombinu ya afya, ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya, ongezeko la vifaa tiba katika ngazi zote za kutolea huduma kuanzia ngazi ya chini mpaka taifa” Alisema Mhe. Senyamule

Aidha, Mhe. Senyamule ameipongeza MSD kwa kuratibu mikutano hiyo ya wadau, kwani vikao hivyo ni daraja muhimu katika kuboresha mahusiano na mawasiliano baina ya pande hizo, kuwapa uelewa wadau namna MSD inavyofanya kazi na mifumo iliyopo, kudumisha umoja na kuwahudumia wananchi kwa wakati, kupeana mrejesho wa huduma zinazotolewa, kuainisha changamoto zinazojitokeza kwenye mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya na kuhakikisha zinapatiwa majibu ili kuleta tija.

Katika hatua nyingine, Mhe. Senyamule ametoa rai kwa watendaji wa sekta ya afya kuvisimamia vyema vituo vya kutolea huduma ili waweze kukusanya mapato ya kutosha, kusimamia thabiti mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya kwa kuepusha upotevu wa bidhaa, ikiwa ni sambamba na kufanya maoteo kwa usahihi na wakati ili kuisaidia MSD kutekeleza wajibu wake kwa weledi na kuleta tija kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai, ameeleza hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na MSD ili kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, ikiwemo mabadiliko ya muundo wa taasisi, maboresho ya maeneo ya uhifadhi wa bidhaa, matumizi ya mifumo ya tehama, mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi, maboresho ya mikataba ya wazalishaji na washitiri, Ongezeko la watumishi ili kukidhi mahitaji, na uanzishaji wa kampuni tanzu kwa ajili ya kusimamia viwanda.

Mavere amesema hivi sasa MSD imepiga hatua kubwa katika kutimiliza mahitaji ya wateja, kwani mnamo mwaka 2022 uwezo wa MSD kutimiza mahitaji na maombi ya wateja ilikuwa asilimia 52 ambapo hivi sasa, uwezo huo umepanda hadi kufikia asilimia 84, huku akibainisha kwamba mkakati na malengo yaliyopo hivi sasa ni kuvuka hapo walipo na kuweza kuwahudumia wateja kwa asilimia 90.

Mavere ametumia fursa hiyo kuwaasa watendaji na wadau wa MSD kuishirikisha MSD katika mipango yake ya ununuzi ya kila mwaka, ili kuhakikisha kwamba Bohari ya inaweza kutimiza mahitaji yao pale wanapohitaji bidhaa hizo, kuliko utaratibu ulipo hivi sasa kwa wateja kuleta mahitaji ya dharura ambayo hayakuwa kwenye mpango wa manunuzi wa MSD wa Mwaka.

About MSD

Medical Stores Department (MSD) was established by the Act of Parliament No.13 of 1993 as an autonomous department under the Ministry of Health, Community Development, Gender, Elderly and Children responsible for developing, maintaining and managing an efficient and cost effective system of procurement, storage and distribution of approved medicines and medical supplies required for use by all public health facilities.