Wazalishaji Bidhaa za Afya Kutoka Jamhuri ya Ucheki, Waitembelea MSD
Wajumbe wa chama cha viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya kutoka Jamhuri ya Ucheki (Czech) ambao wako ziarani nchini Tanzania wametembelea Bohari ya Dawa (MSD) na kuelezea maeneo mbalimbali wanayoweza kushirikiana na Tanzania hasa upande wa bidhaa afya.
Wajumbe hao ambao wamefuatana na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambaye pia anahusika na Jamhuri ya Ucheki (Czech) Dkt. Abdallah Possi wameeleza kuwa ziara yao nchini Tanzania ina lengo pia la kuimarisha mahusiano ya kidoplamasia na kuangalia maeneo ya ushirikiano upande wa bidhaa za Afya ambazo ni pamoja na dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara.
Kwa mujibu wa Rais wa Chama hicho Petr Foit, idadi kubwaya viwanda nchini mwao imejikita zaidi kuzalisha bidhaa za afya, hivyo ni vyema wakajua Tanzania ina uhitaji wa bidhaa za aina gani ili kuweza kushirikiana katika hilo.
Ujio huo pia umeonesha nia ya kuipatia Tanzania bidhaa za kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwa ni pamoja na Ebola, ambapo Wizara ya Afya kupitia MSD watakaa na kuainisha mahitaji hayo,na kuwasilisha kwa Rais wa Umoja huo wa wazalishaji ili kufanya utaratibu wa kupata bidhaa walizonazo.
- Log in to post comments