MSD Yakutana na Wataalamu wa Maabara Nchini.
Bohari ya Dawa (MSD), imekutana na wataalam wa maabara ambao ni Mameneja wa maabara za hospitali za Rufaa za Mikoa,Maalum,Kanda na Taifa. Kikao hiki kinachofanyika kwa siku tatu mkoani Dar es Salaam lengo lake ni kutathimini upatikanaji na ubora wa bidhaa za afya za maabara zinazosambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, amewaeleza washiriki kuwa watumie siku hizi tatu zilizopangwa kuhakikisha wanakuja na majawabu ya changamoto zinazojitokeza katika sekta hii ya maabara.
“ Tunaweza kutumia Sekta hii ya Maabara kuwa ya kibiashara na kuongeza mapato ya hospitali zetu huku tukiboresha huduma zinazotolewa kupitia sekta hii ya maabara” alisema Mavere.
Mavere aliongeza kuwa tunachotaka ni kuwa na utaratibu wa pamoja na uwazi kwani nje ya kufanya hivyo kuna watu hawataelewa kama bidhaa fulani ipo eneo fulani. Tunataka kupunguza ile hali ya vitendanishi kuisha muda wake kabla ya kutumika ilhali kuna maeneo vilikuwa vinahitajika ila tu hawakuwa wanajua.
Naye Kaimu Mfamasia Mkuu wa serikali, Msafiri Chiwanga, alisema serikali imeendelea kuwekeza katika mashine za kiuchunguzi ili kuhakikisha mgonjwa anapatiwa tiba sahihi kulingana na ugonjwa unaomsumbua kupitia kwa wataalamu wa maabara.
Chimwaga aliongeza kuwa , kufuatia kuwepo kwa changamoto za usugu wa vimelea vya magonjwa katika baadhi ya dawa, wataalamu wa maabara wanatajwa kuwa msaada katika kuhakikisha tiba inayotolewa kwa mgonjwa inaendana na ugonjwa husika na hii ni baada ya matokeo ya vipimo kupitia mashine za kiuchunguzi.
- Log in to post comments