Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi MSD, Watembelea Mbuga ya Taifa ya Tarangire
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Bohari ya Dawa (MSD) wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Tarangire lengo likiwa ni kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika hifadhi hiyo ambayo inapatikana ndani ya mkoa wa Manyara.
Ziara hiyo imekuja ili kuongeza chachu na kuhamasisha wageni na watumishi mbalimbali kuweza kutembelea vivutio vyetu vya utalii vilivyoko nchini, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Kutangaza utalii nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Katibu wa Baraza hilo Bi. Joan Ruth Msangi amesema kuwa wao kama wawakilishi wa watumishi wa MSD, wanaishukuru Menejimenti ya MSD kwa kuwezesha safari hiyo na wamemeona fahari kutembelea mbuga hiyo yenye vivutio vya kipekee ambavyo ni adimu kuviona katika maeneo mengine.
“Hifadhi ya taifa ya Tarangire ina wanyama wengi, ikiwemo makundi makubwa ya Tembo, ambapo hii leo tumepata bahati ya kuwaona ikiwa ni fursa ya kipekee kwetu sisi watumishi wa MSD kujionea wanyama hao tena kwa ukaribu zaidi” alisema Msangi
Kwa upande wa wafanyakazi waliotembelea hifadhi hiyo, wamepongeza jitihada zilizofanywa na viongozi wa MSD kuhakikisha safari hiyo inafanikiwa na kuwataka viongozi na watumishi wa taasisi nyingine kutembelea hifadhi hiyo ya kipekee na nyinginezo zinazopatikana nchini, ili kutalii, kujifunza na kuelimika juu ya masuala mbalimbali ya uhifadhi.
Hifadhi ya taifa ya Tarangire ni hifadhi ya sita kwa ukubwa Tanzania, inayopatikana Mkoani Manyara, ikiwa na ukubwa kilometer za mraba 2,600.
- Log in to post comments