Skip to main content
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Akiwa na Wajumbe wa Kikao cha Wadau na Wateja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam

Viongozi wa Sekta ya Afya Wahimizwa Kushirikiana na MSD

MOROGORO.

Wasimamizi na wadau wa afya mkoani Morogoro, wameaswa kushirikiana kwa ukaribu na Bohari ya Dawa (MSD), ili kwa pamoja waweze kutatua na kuboresha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya mkoani humo, kwa ajili ya ustawi watu na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa hii leo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wà Morogoro, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini Mhe. Rebeka Nsemwa, wakati akifungua kikao kazi cha wateja na wadau wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, kilichokutanisha viongozi wa sekta ya afya ngazi ya mkoa na wilaya mkoani humo.

“Mkoa huu una jumla vya vituo 378 vya kutolea huduma za afya ambavyo vinajumuisha hospitali kumi na sita(16), ikiwemo hospitali mbili za rufaa, vituo vya afya arobaini na sita (46) na zahanati mia tatu kumi na sita (316), hivyo fanyeni kazi kwa pamoja na kujadiliana namna bora ya kuboresha utekelezaji wa majukumu yenu, na hata kupeana mrejesho wa masuala mbalimbali yanayohusiana na mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya.” Alisisitiza Mhe. Nsena

Mhe. Nsemwa amewataka viongozi hao kuhakikisha wanakuwa na majadiliano yenye tija kwa kuainisha namna bora ya kufanya kazi kwa pamoja, badala ya kutupiana lawama na kunyosheana vidole, ili kila upande uweze kutimiza wajibu wake katika kuwahudumia wananchi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Nsemwa amewataka watendaji hao kuboresha maoteo yao ya bidhaa za afya, kwenye vituo wanavyosimamia kila mmoja katika eneo lake, ili kuepukana na sintofahamu ya ukosefu wa bidhaa za afya vituoni, inayosababishwa na taarifa zisizosadifu mahitaji halisia.

Watalamu hao wa afya pia wametakiwa kusimamia matumizi sahihi ya bidhaa za afya, kwa kila mmoja ana wajibu wa kusimamia matumizi sahihi ya bidhaa za afya, ili kuleta tija kwa wananchi, kwani serikali imekuwa ikiongeza na kutenga bajeti ya dawa na vifaa tiba ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.

Aidha, Mhe. Nsemwa amewahimiza watendaji hao kulipa na kupunguza madeni yao wanayodaiwa na MSD, ili kuiongezea MSD uwezo wa kuwahudumia wateja wake, kutokana na vituo hivyo vya kutolea huduma za afya, kuwa na limbikizo la madeni, hivyo kuathiri utendaji wa MSD.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amewasilisha mchakato wa maboresho mbalimbali ya huduma za MSD, kwa kuainisha hatua mbalimbali zilizofikiwa kwenye maboresho ya huduma, na utendaji,huku akiahidi kufanyia kazi yale yote yaliyoibuliwa ndani ya kikao hicho ili kwa pamoja kuweza kuboresha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.

Tukai pia ameainisha jinsi MSD ilivyojikita katika mchakato wa uanzishaji wa viwanda mbalimbali vya bidhaa za afya nchini, mathalani viwanda vya barakoa, mipira ya mikono,na viwanda vya bidhaa za pamba ili kuondoa utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dar es salaam, Betia Kaema, amewashukuru Wadau hao kwa kuitikia wito na kuhudhuria kikao hicho kwani imeonyesha ni jinsi gani wadau hao walivyo na kiu ya kuboresha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya mkoani humo, hivyo kuahidi kuchukua ushauri na maoni yao ili kuboresha utendaji wa Kanda hiyo.

About MSD

Medical Stores Department (MSD) was established by the Act of Parliament No.13 of 1993 as an autonomous department under the Ministry of Health, Community Development, Gender, Elderly and Children responsible for developing, maintaining and managing an efficient and cost effective system of procurement, storage and distribution of approved medicines and medical supplies required for use by all public health facilities.