Tanzania Yapokea Msaada Kutoka Benki ya TDB
DAR ES SALAAM:
Serikali ya Tanzania, imepokea msaada wa shilingi milioni 230 kutoka Benki ya Biashara na Maendeleo (TDB) kwa ajili ya kununulia vifaa vya kujikinga na kupambana na ugonjwa wa Uviko-19.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Uongozi wa benki hiyo, Mkurugenzi wa Uhusiano na Uwekezaji Bi. Mary Kamari, amesema benki yake imetoa msaada huo ili kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko 19, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika miradi mbalimbali kimkakati ili kuwaletea Watanzania maendeleo.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya serikali, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), ameipongeza benki hiyo kwa mchango wake kwa sekta ya afya, huku akiisihi kuendelea kushirikiana na serikali kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe amesema Wizara imepokea msaada huo kwa unyenyekevu mkubwa kwani utasaidia katika mapambano ya milipuko ya magonjwa yanayoshabihiana na Uviko-19 mathalani mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, uliozikumba nchi jirani.
- Log in to post comments