Rais Samia Apeleka Tabasamu Kwa Wananchi wa Kata ya Magazini - Wilaya ya Namtumbo
Kituo cha Afya cha Magazini kilichopo Kata ya Magazini Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kimepata msaada wa vifaa Tiba vya kisasa vya upasuaji vikiwemo vya wamama wajawazito vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 100 ili kuweza kusaidia kuboresha huduma za afya kwenye kata hiyo, iliyoko mpakani na nchi ya msumbiji .
Akielezea utendaji kazi wa vifaa Tiba hivyo Meneja wa Bohari ya Dawa (MSD) kanda ya Iringa Robert Lugembe alisema kuwa vifaa hivyo vitawasaidia watu wengi ambao kwa sasa baadhi yao wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa yanayohitaji upasuaji ikiwemo akina mama wajawazito.
Lugembe alisema kuwa serikali italeta tena vifaa Tiba vya kisasa vingine vyenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 100 na kwamba MSD wataendelea kupeleka vifaa tiba hivyo vya kutosha mpaka pale kituo hicho kitakaposheheni vifaa kwa ajiri ya kuendelea na kazi.
"Nilikuwa naangalia hapa nikasema katika hii migao ya serikali inayoendelea hamna Jenereta, lakini hapa Jenereta linahitajika sana, kwa hiyo MSD tutaleta Jenereta ambalo litasaidia kwenye shughuli za upasuaji." Alisema meneja huyo wa Kanda ya Iringa Rugembe.
Alivitaja Vifaa hivo kuwa ni pamoja na kitanda maalum cha kufanyia upasuaji (operating table), taa ambayo inatoa mwanga wakati zoezi la upasuaji linaendelea(Operating light), vifaa vya uchunguzi, mashine ya kutakasa vifaa , mashine ya kufulia nguo, mashine vya kukaushia vyombo, pamoja na vifaa vya upasuaji vya kutosha vyote vikiwa na hamani ya zaidi ya sh.milioni 100.
Awali akipokea msaada huo mganga Mkuu wa kituo cha Afya cha Magazini Dkt.Rashid Athuman alisema kuwa kituo hicho toka kianze kufanya kazi hakijawahi kutoa huduma za upasuaji lakini kwa sasa amedai vifaa tiba hivyo vitasaidia kutumia teknolojia ya kisasa zaidi ambayo itamfanya mgonjwa kurejea afya yake kwa haraka zaidi.
Dkt. Athuman alisema kuwa kituo hicho cha Afya cha Magazini kina malengo na mikakati ya kuhakikisha kwamba inatoa huduma bora ambazo wananchi wenye kipato duni wanaweza kuzifikia na kuzimudu na si vinginevyo.
"Tunatoa shukrani zetu kwa serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa ushirikiano tunaopewa na MSD tunaomba ushirikiano huu uendelee kudumishwa kwa mtazamo wa kwamba lengo letu ni moja, na wajibu wetu ni mmoja kwaajiri ya kuhudumia wananchi hasa hawa waliopo mipakani na nchi jirani ya Msumbiji" alisema Dkt. Athuman.
Awali akisoma taarifa fupi ya kituo hicho cha Afya Mtendaji wa kata ya Magazini Mussa Ponera alisema kuwa kituo hicho kilianzwa kujengwa 2019/2020 ambapo walipokea fedha kutoka serikali kuu kiasi cha sh. Milioni 500 na kwamba hadi Sasa wanahitaji kiasi cha sh. Milioni 120 ili kukamilisha miundombinu ya vyoo, mahabara, jengo la upasuaji pamoja na jengo la mama na mtoto.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mhe.Vita Kawawa ameishukuru serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa lengo na mikakati ya kuhakikisha kwamba inatoa huduma bora ambazo wananchi wenye kipato duni wanaweza kuzifikia na kuzimudu.
Alisema kuwa zoezi la serikali kugawa vifaa tiba vya kisasa kutoka MSD litaendelea kufanyika ili kufikia lengo la kutoa huduma iliyokuwa bora zaidi kwa wagonjwa na kuondokana na wimbi kubwa la baadhi ya wagonjwa kwenda umbali mrefu kutibiwa kwa ukosefu wa baadhi ya vifaa kwenye vituo vya Afya vilivyopo Jimbo la Namtumbo.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo ya Magazini Grace Kapinga alisema kuwa msaada huo wa vifaa tiba vya upasuaji utawarahisishia wananchi kutembea kilometa 202 kwenda kufuata huduma za upasuaji hospital ya Mkoa Songea (HOMSO)jambo ambalo akina mama wajawazito wengi wamepoteza maisha kwa kukosa huduma hizo za upasuaji.
Kwa upande wao wananchi wa kata hiyo Amina Ally na Awetu Kassim, wameipongeza na kuishukuru serikali kwa kuwaletea vifaa tiba kwani walikuwa wanapata shida hasa kwa kukosekana kwa vifaa vya upasuaji katika kituo hicho cha Afya.
Wamesema , pamoja na kuletewa vifaa hivyo wameiomba serikali kupeleka huduma ya umeme ambapo tayari nguzo na nyaya zimeshawekwa bado kuingiza kwenye majengo ili vifaa hivyo viweze kutumika kama ilivyokusudiwa kwani haitaleta maana vifaa vimeletwa lakini havitumiki kwa kukosa huduma ya umeme.
- Log in to post comments