Mtendaji Mkuu Global - Fund, Atembelea MSD
Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Dunia (Global fund) Bw. Peter Sands, amefanya ziara Bohari ya Dawa (MSD) na kujionea namna MSD inavyotekeleza majukumu yake.
Kupitia ziara hiyo, Mtendaji Mkuu huyo, amepata wasaa wa kutembelea maghala ya kuhifadhia bidhaa za afya, yanayomilikiwa na MSD, yaliyoko Keko, jijini Dar es Salaam.
Bwana Sands ameahidi kuwa mfuko huo utaendelea kuiwezesha MSD kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya, hasa za miradi Msonge, huku akiipongeza MSD kwa kufanikisha usambazaji wa vyandarua nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Mavere Tukai amemshukuru Bw. Sands kwa kuendelea kushirikiana na MSD katika nyanja mbalimbali za mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, huku akibainisha maboresho mbalimbali yanayofanywa MSD kwasasa kuwa ni pamoja na kuimarisha uhifadhi kwa kuongeza maghala, kuimarisha mifumo ya uhifadhi, tehama na kuongeza baadhi ya watumishi katika kada mbalimbali kulingana na mahitaji ya majukumu ya MSD.
Ameongeza kuwa, maeneo mengine ni pamoja na kuimarisha manunuzi ya bidhaa za afya, ufuatiliaji pamoja na uwezo wa kuchambua na kuchakata taarifa, sambamba na ukuzaji wa mtaji wa MSD.
Katika hatua nyingine, Mavere amebainisha kwamba MSD imeendelea kufanikiwa katika ununuzi na usambazaji wa bidhaa za miradi misonge, sambamba na kufanyia kazi hoja mbalimbali zilizo ibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa mfuko huo.
- Log in to post comments