MSD Yazindua Kampeni ya Usambazaji Vyandarua Ngazi ya Kaya - Mkoa wa Tabora
MKOA wa Tabora umetajwa kuwa wa kwanza kitaifa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria hali inayotokana na imani potofu ya matumizi ya vyandarua vyenye dawa kuwa vinapunguza nguvu za kiume.
Takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria kimeongezeka kutoka asilimia 11.7 mwaka 2016/2017 hadi asilimia 23.4 mwaka 2022 wakati kiwango cha maambukidhi ya malaria kitaifa ni asilimia 8.1.
Kutokana na hali hiyo serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imetia kambi mkoani humo na kusambaza vyandarua vyenye dawa.
Akizungumza jana Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Luis Bura, amesema hali ya ugonjwa wa malaria ni mbaya mkoani humo ambapo unaongoza kwa maambukizi nchini.
“Tafiti zinaonyesha kiwango cha maambukizi ugonjwa wa malaria kwa mwaka 2016/2017 kwa watoro wa umri wa miezi sita hadi miaka 5 ni asilimia 20 na mwaka 2018 yameongezeka kufikia asilimia 23,” alisema.
Alieleza kuwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo kitaifa ni asilimia 8.1 hivyo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 11.7 hali inayosababisha mkoa huo kuongoza.
Alisema hali hiyo haikubaliki hivyo ni lazima kuwa na nguvu ya pamoja kwa watendaji na jamii kuhakikisha maambukizi hayo yanapungua.
Bura alisisitiza, makundi ambayo yako hatarini ndio yatanufaika na vyandurua hivyo wakiwemo watoto chini ya miezi tisa na miaka mitano, wajawazito, wanafunzi , wazee wa miaka 60 na watu wanaoishi na VVU.
Alisema, zaidi ya kaya 300,000 kati ya kaya 400,000 ambazo zitapewa vyandarua hivyo ambavyo ni zaidi ya milioni 1.8.
Naye Kaimu Meneja wa MSD Tabora Adonizedeck Tefurukwa, alishukuru uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini na kuwahakikishia wananchi wa Tabora kuwa, kila mnufaika wa vyandarua hivyo atafikiwa.
Alisema katika usambazaji huo wamejipanga ipasavyo na wanatimu ya kutosha kufika katika kila maeneo na ili kufanikisha hatua hiyo, wamekodisha maghala mawili ya ziada eneo la Nzega na Igunga.
“ Katika usambazaji huo tumepokea zaidi ya vyandarua milioni 1.8 ambavyo vitasambazwa katika vituo 2,673 sawa na Kaya zaidi ya 400,000,”alisema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Honoratha Rutatinisibwa, alisema takwimu hizo zinatokana na mkoa huo wananchi wake kuwa na imani potufu ya matumizi ya vyandarua vyenye dawa kuwa vinapunguza nguvu za kiume.
Pia kuwa na usafi wa mazingira usioridhisha, halmashauri kushindwa kutenga bajeti ya ununuzi wa viwadudu, wananchi kutokuwa na mwamko wa kupima na mkoa huo kutoingizwa katika mpango wa taifa qa kupulizia dawa za ukoko
“Bila kusahau ongezeko la mazali ya mbu yanayotokana na kilimo, jiografia ya mkoa kuwa na maeneo mengi yenye madimbwi ya naji yaliyotuama na kutokuwa na wadau wanaotoa misaada ya afua za kupambana na ugonjwa huo,” alisema.
- Log in to post comments