MSD Yateta na Wazalishaji, Wasambazaji na Washitiri wa Bidhaa za Afya.
Bohari ya Dawa (MSD) imekutana na wazalishaji, wasambazaji na washitiri wa bidhaa za afya zaidi ya 200 kutoka nje na ndani ya nchi kujadiliana namna ya kuboresha ushirikiano na kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.
Katika hafla hiyo Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewaeleza wadau hao kuwa serikali inaendelea kuboresha ushirikiano na sekta binafsi kuchagiza uanzishaji wa viwanda vya bidhaa za afya nchini.
Nia kubwa ni kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kununua bidhaa za afya kutoka nje ya nchi, ambapo kwa sasa asilimia 85 ya bidhaa hizo zinatoka nje ya nchi.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu ameeleza kuwa ofisi yake ipo tayari kuiunga mkono MSD katika uanzishwaji wa viwanda vya bidhaa za afya kwa kushirikiana na sekta binafsi, kwani ni miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele na serikali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD Rosemary Silaa amesema kukaa na wadau na kujadiliana ni jambo muhimu katika kuboresha huduma, huku Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai akieleza kuwa mifumo ya ununuzi imeboreshwa ikiwa ni pamoja na kuingia mikataba ya muda mrefu na wazalishaji.
- Log in to post comments