MSD Yapongezwa Kuanzisha Mikutano na Wadau Wake
Dodoma.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Ally Senga Gugu, ameipongeza Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dodoma kwa kukutana na wadau wake na kujadili masuala mbalimbali yahusuyo mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, yanayogusa pande zote mbili kwa lengo la kuboresha huduma na kuleta tija kwa wananchi.
Mhe. Gugu ametoa pongezi hizo hii leo, wakati akifungua kikao kazi baina ya MSD Kanda ya Dodoma na wadau wake wa Mkoa wa Dodoma, kilichofanyika wilayani Kondoa, kwa lengo la kujadili mafanikio, maboresho na changamoto mbalimbali zilizopo baina ya pande hizo mbili.
Bw. Gugu ameongeza kuwa mkutano huo ni daraja muhimu la kuhakikisha MSD na wadau wake wanadumisha umoja ambao utawawezesha kuwahudumia wananchi kwa wakati, kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake, sambamba na kupokea changamoto zitakazoibuliwa na kuzipatia tatuzi ili kuboresha huduma za afya.
“Hakikisheni kunakua na majadiliano yenye tija ya namna bora ya kufanya kazi kwa Pamoja ili kila mmoja aweze kutimiza wajibu wa kumhudumia mwananchi. Ni mategemeo yangu baada ya Mkutano huu tutaondoka na uelewa wa Pamoja na maadhimio, ambayo utekelezaji wake utaboresha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya na kuboresha huduma.”_ alisema Bw. Gugu.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Best Magoma, amewataka madaktari na watalaamu wote waliohudhuria Mkutano huo, kujadili kwa uwazi changamoto mbalimbali zinazowakabili, ili kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, kwani suala hilo ni mtambuka linalohitaji juhudi za pamoja ili kuepuka lawama zisizo za lazima baina ya MSD na wadau wake.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Bw. John Sipendi, amewashukuru wadau wake kwa kuitikia wito wa kushiriki mkutano huo, huku akianisha mikakati na maboresho mbalimbali inayotekelezwa na MSD kwa sasa, ili kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa bidhaa za afya. Aidha ameomba wadau hao kuendeleza mahusiano na mawasiliano wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao, ili kuongeza tija katika kuhudumia wananchi.
- Log in to post comments