MSD Mfano wa Kuigwa SADC
Wakuu wa Taasisi za Bohari ya Dawa pamoja na viongozi wanaosimamia manunuzi ya bidhaa za afya katika Jumuia ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wameeleza kuwa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) imekuwa mfano wa kuigwa katika nchi za jumuiya hiyo.
Aidha wamesema MSD itakuwa chachu ya kuunganisha maendeleo na kukuza uchumi wa Afrika kutokana na ufanisi wake katika upatikanaji wa uhakika wa dawa na bidhaa za afya.
Akizungumza leo Julai 12, 2023 jijini Dar es Salaam baada ya kufanyika kwa mkutano wa siku mbili kwa viongozi hao uliofanyika nchini Tanzania Mwenyekiti wa wakuu hao Richard Biayi amesema wameona shughuli zinazofanywa na MSD na wameridhishwa nayo na wanaamini siku chache zijazo Afrika itashikamana hasa katika eneo la uagizaji bidhaa za afya.
Ameongeza wakiwa MSD wametembelea ghala la kuhifadhi dawa na bidhaa za afya sambamba na kushuhudia uzalishaji wa barakoa kwenye kiwanda cha MSD kilichopo kwenye bohari hiyo na walichojifunza Tanzania imepiga hatua kwenye eneo hilo kupitia MSD.
Viongozi hao wapo nchini tangu Julai 10 kwa ajili ya kikao cha kujadili na kuboresha namna ya kununua dawa kinachotarajiwa kumalizika leo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai ameeleza kuwa uwepo wa viongozi hao kutoka jumuiya ya SADC imelenga kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu maboresho ya kimifumo katika uendeshaji bohari ya dawa.
"Ni kama tunabadilishana uzoefu na kila mmoja anajifunza, mfano wenzetu Zambia ni wazuri sana kwenye nishati mbadala kwa hiyo ni vema kujifunza ili nasi siku zijazo tupunguze gharama," alisema.
Ameongeza mkutano wao wa mkakati wa manunuzi dhidi ya viongozi hao wa SADC ulihudhuriwa na nchi zote za Jumuia hiyo na ambao hawakuwepo walishiriki kwa njia ya mtandao na wametoka na mapendekezo kadhaa.
"MSD na secretarieti ya SADC tumejadili namna ya kuboresha manunuzi na tumetoa mapendekezo ta muda mfupi, wakati na mrefu.” amesema.
Aidha amesema wamependekeza namna ya kuboresha mfumo wa manunuzi na kuboresha bidhaa za afya, usimamizi, rasilimali watu na fedha, malipo na mawasiliano.
“Mfano mfumo unatakiwa wa kidigitali maana tuko nchi mbalimbali hatuwezi kuwasiliana kwenye makaratasi na mapendekezo yakikubaliwa, vipaumbele vitawekwa na tutakwenda kwenye utekelezaji,” amesema Tukai.
- Log in to post comments