MSD Kusambaza Vyandarua Milioni.1.55 Mkoa wa Shinyanga
Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) inatarajia kusambaza jumla ya vyandarua milioni moja na nusu, kwa wananchi katika ngazi ya kaya Mkoani Shinyanga, ikiwa ni kampeni maalum yenye lengo la kupambana na kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini.
Hayo yameelezwa leo februari 8,2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa MSD Bw.Victor Sungusia, wakati wa uzinduzi zoezi la kusambaza vyandarua mkoani humo, kupitia kampeni maalum (TMC) chini ya mpango wa taifa wa kudhibiti malaria nchini(NMCP).
Sungusia amesema MSD imekuwa na uzoefu wa muda mrefu kwenye usambazaji wa bidhaa za afya, hivyo watatekeleza jukumu hilo kwa weledi na ufanisi mkubwa katika muda uliopangwa.
"Kama yalivyo majukumu yetu kwa mujibu wa Sheria, kazi yetu ni kuzalisha, kununua,kutunza na kusambaza bidhaa za afya nchini, na hicho ndo kilichotuleta hapa leo, neti tayari zimekwisha nunuliwa na zipo za kutosha, zinasubiri tu kusambaza" alisema Sungusia
Sungusia ameongeza kwamba MSD ina miundombinu wezeshi ikiwemo magari ya kutosha na madereva wenye weledi wa hali ya juu, ambao wako tayari kutekeleza usambazaji huo.
"Tunategemea kusambaza neti hizi katika Halmashauri zote sita za mkoa huu, na tuna vituo zaidi ya 600 mkoa mzima, na kazi hii tutaifanya kwa siku 10 tu, hivyo tuko tayari kusambaza". Alisisitiza Sungusia.
Sungusia amewaomba viongozi na wananchi wa mkoa wa Shinyanga kila wilaya kuanzia ngazi ya juu hadi chini, kuipa MSD ushirikiano ili waweze kumaliza zoezi hilo katika muda uliopangwa.
Aidha, amewahakikishia wananchi wote wa mkoa huo waliojiandikisha kuwa watapata vyandarua vyao, kwani MSD itafanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa, na hadi sasa MSD imekwisha pokea vyandarua vyote vinavyohitajika katika Mkoa huo, hivyo waondoe shaka.
Awali akizundua rasmi zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka wananchi wa Mkoa huo kuzingatia matumizi sahihi ya vyandarua Ili dhima ya serikali katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria iweze kutimia, badala ya kutumia vyandarua hivyo katika matumizi yasiyofaa kama kufugia kuku, au kuvulia samaki.
Aidha ameitaka jamii kuondokana na imani potofu kwamba vyandarua hivyo vinapunguza nguvu za kiume, kwani suala hilo sio la kweli, na lilianzishwa na watu wenye nia ovu, hivyo kuwataka wananchi kutumia vyandarua hivyo kwani ni salama
- Log in to post comments