MSD KUSAMBAZA VIDONGE MIL. 22 VYA VITAMINI A NCHINI
Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameikabidhi Serikali ya Tanzania kupitia kwa Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel kwa niaba ya Waziri ya Afya Mhe. Ummy Mwalimu vidonge milion 22 vya matone vya Vitamini A kwa ajili ya watoto, vilivyotolewa na serikali ya Canada, kupitia shirika la Nutrition International (NI).
Dkt. Kikwete, amekabidhi dawa hizo akiwa mmoja wa wajumbe wa bodi wa Shirika la kimataifa la Nutrition international ambalo ndio limetoa msaada huo.
Akikabidhi dawa hizo ameeleza kuwa lengo ni kuwasaidia watoto na dawa hizo zitatolewa kwa awamu mbili yaani mwezi Juni na Disemba kwa watoto takribani milioni 11 walio chini ya umri wa miaka mitano.
Dkt. Kikwete ameeleza kuwa vitamini A husaidia kuimarisha afya ya macho na kuongeza kinga ya mwili kwa mtoto hivyo ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha watoto wanapatiwa matone haya.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali kupitia Wizara afya inashukuru na imepokea vidonge vya matone ya Vitamini A milioni 22 kutoka kwa shirika la Nutritrion International, ambayo itasaidia watoto milioni 11.
Aneongeza kuwa elimu ya mtoto inaanza tangu siku mimba inatungwa, kwa kumpatia Mama lishe bora wakati wa ujauzito ili kusaidia kuimarisha ubongo wa mtoto, hivyo amewakumbusha wazazi kuzingatia lishe bora kwa watoto tangu wa utangaji wa mimba na kuwa na desturi ya kula mlo bora kwa mama wajawazito.
Dawa hizo zimehifadhiwa Bohari ya Dawa (MSD) na zitasambazwa kwa kuzingatia mgawo utakaotolewa na Wizara ya Afya katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
MSD imekuwa msambazaji mkuu wa dawa hizo na nyingine kadha wa kadha kwa kuhakikisha dawa hizo zinawafikia wananchi kupitia vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya nchini, zahanati na hospitali.
- Log in to post comments