MSD Kuja na Suluhu ya Special Procurement
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, ambaye pia ni mlezi wa Kanda ya MSD Kagera Bi. Rosemary Slaa, amewahakikishia wataalamu wa afya kutoka Mikoa ya Kagera na Geita kuwa Bohari ya Dawa (MSD) inaendelea kufanya maboresho katika upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, mathalani upatikanaji wa vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa wakati.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ametoa kauli hiyo leo, Mkoani Kagera, wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha MSD Kanda ya Kagera na wadau wake kutoka mikoa ya Kagera na Geita, (waganga wakuu wa Mikoa, Wilaya/halmashauri, Wafamasia na Wataalamu wa maabara wa mikoa na wilaya) waliokutana kujadili changamoto mbalimbali zinazoukabili mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya kwenye kanda hiyo na tatuzi zake.
“Tumelivalia njuga suala la Special Procurement, kwa kuweka mikakati ya kuhakikisha tunakuwa na bidhaa hizo ndani ya Bohari, hasa bidhaa ambazo zimekuwa zikiombwa mara kwa mara na tayari tumeagiza shehena kubwa, hivyo muda si mrefu baadhi ya bidhaa hizi zitaanza kupatikana na kuondoa kusubiri bidhaa hizo kwa muda mrefu.” alisema Bi. Rosemary.
Ameongeza kuwa wanaipongeza serikali ya awamu ya Sita, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuazimia kuipatia mtaji MSD, kwani hatua hiyo itasaidia MSD kujitegemea, na kuongeza uwezo wake wa kuhudumia wateja wake.
Naye Meneja wa MSD kanda ya Kagera Bw.Kalendero Masatu amedokeza kwamba, yapo mategemeo ya kuwa na ongezeko la upatikanaji wa dawa kwa asilimia 70 hadi 80, kwani tangu mwezi julai mwaka jana hadi kumalizika mwezi June 30 mwaka huu, upatikanaji wa dawa uliongezeka kwa asilimia 65 kwenye robo ya nne kutoka 55 ya robo ya kwanza.
Bw. Masatu amewashukuru wadau hao kwa kukubali wito na kuhudhuria kikao hicho, na kuahidi kufanyia kazi maazimio yote yaliyo adhimiwa huku akisisitiza ushirikiano na mawasiliano ya mara kwa mara na wadau hao
- Log in to post comments