Mkuu wa Wilaya ya Igunga Apongeza Maboresho ya Huduma za MSD
Mkuu wa Wilaya ya Igunga Mhe. Sauda Salum Mtondoo ameipongeza Bohari ya Dawa MSD kwa maboresho ya huduma zake, hali ilipelekea upatikanaji wa uhakika wa bidhaa za afya nchini, hivyo kuleta unafuu wa huduma kwa watoa huduma na wananchi kwa ujumla wilayani humo.
Mhe. Mtondo ametoa salamu hizo hapo jana kwenye kikao kazi, kufuatia ziara ya Ujumbe wa MSD ukiongozwa na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya MSD Dkt. Rashid Mfaume, aliyeongozana na Kaimu Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji MSD Bw. Victor Sungusia Pamoja na Wajumbe wengine kutoka Kanda ya MSD Tabora, kutembelea wilaya hiyo, kwa ajili ya kutathimini hali ya utoaji wa huduma za MSD Mkoani Tabora.
Mhe. Mtondo amebainisha kwamba, Hivi sasa MSD imejitahidi kwenye eneo la upatikanaji wa bidhaa za afya ukilinganisha na huko nyuma na kufanya adha ya ukosefu wa bidhaa za afya vituoni kupungua kwa kiasi kikubwa, hivyo kuondoa malalamiko ya wananchi yaliyokuwepo awali.
Aidha, ameitaka MSD kutobweteka bali kuongeza juhudi zaidi ili kuhakikisha pengo lililobaki kwenye upatikanaji wa baadhi ya bidhaa za afya hasa vifaa tiba, linamalizika hivyo kufanya uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika kujenga na kubboresha miundombinu ya sekta ya afya, ikiwa ni Pamoja na uwepo wa watumishi kuleta tija.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Dkt. Mfaume ameipongeza Halmashauri ya Igunga kwa uwekezaji katika miundombinu ya sekta ya afya, Pamoja na huduma za afya kwa ujumla, huku akibainisha kwamba MSD inaendelea na maboresho ya huduma zake, ili kuhakikisha inakidhi malengo yaliyokusuidiwa ya kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji tosheelevu wa bidhaa za afya nchini.
Ameongeza kuwa MSD itaendelea kuboresha mawasiliano na uhusiano kwa wateja na wadau wake, ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa Pamoja, sambamba na kufahamu michakato na hatua mbalimbali ambazo MSD inazichukua, katika kuhakikisha inaboresha huduma zake, ili kwa pamoja waweze kuboresha hali ya utoaji wa huduma za afya nchini.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Luciana Kafumu, amesema hali ya upatikanaji wa Dawa na Vifaa tiba Wilayani humo ni wastani wa asilimia 91%, hatua ambayo imeboresha hali ya utoaji wa huduma, kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wilayani humo.
Aidha, licha ya kuipongeza MSD kwa kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, Dkt. Kafumu ameishauri MSD kuboresha upatikanaji wa baadhi ya vifaa tiba,ambavyo vimekuwa ngumu kupatikana kwa wakati, ili kuweza kukidhi matakwa ya vituo vipya vilivyojengwa na kukamilika, sambamba na kupanua hali ya utoaji wa huduma kwa baadhi vituo vya kutolea huduma.
- Log in to post comments