Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Aonya Matumizi Mabaya ya Vyandarua
#SONGWE
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Dk. Francis Michael, ameonya matumizi mabaya ya vyandarua kama vile kufugia kuku au kuvulia samaki.
Akizungumza jana mkoani humo wakati akizinduza mpango wa ugawaji wa vyandarua katika shule za msingi Dk.Micheal amesisitiza kuwa vitendo hivyo vinaathiri juhudi za Serikali na wadau wa afya katika kupambana na Malaria.
Pia alisema ni utovu wa nidhamu na upotevu wa rasilimali muhimu kwa wananchi kutumia vyandarua hivyo vibaya kwa kufugia kuku au kuvulia samaki hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wanaokiuka agizo hilo.
“Mpango wa ugawaji wa vyandarua kupitia shule za msingi unalenga kufikisha vyandarua kwa familia zote na kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi, lengo ni kupambana na Malaria, hivyo nitoe onyo nikikuta vyandarua hivi vinafugiwa kuku au kuvuliwa samaki nitachukua hatua kali,”alisema.
Dk. Micheal alisisitiza kuwa, dhamira ya serikali ni kuhakikisha kuwa mkoa huo unabaki kuwa mfano wa kudhibiti ugonjwa wa Malaria na wananchi wanakuwa na afya bora hivyo ni muhimu kuwapo na matumizi sahihi ili kuleta mafanikio.
Alisema, kwa sasa Mkoa wa Songwe unajivunia kiwango cha chini cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kilichopo lakini ipo haja jitihada zaidi kuchukuliwa katika kudumisha hali hiyo.
Alisema katika mpango mkakati wa kimkoa uliopo wa kutokomeza ugonjwa huo ni pamoja na kuhakikisha kipaumbele cha kwanza ni ugawaji wa vyandarua vyenye dawa na elimu ya matumizi sahihi ya vyandarua hivyo inakuwaendelevu katika jamii hususani kwa watoto na wafunzi waliopo shuleni.
Kwa upande wake Meneja wa Bohari ya Dawa Kanda ya Mbeya Marco Masala alisema bohari ikiwa ndio wasambazaji wa vyandarua hivyo vya serikali kwa jamii watahakikisha dhumuni linafikiwa.
Aidha alitoa wito kwa jamii kuwa na utayari kwani matumizi ya vyandarua ni muhimu katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria
- Log in to post comments