Maboresho ya Mnyororo wa Usambazaji Bidhaa za Afya Nchini
Ongezeko la usambazaji wa bidhaa za afya unaofanywa na Bohari ya Dawa (MSD) tangu Mwaka wa Fedha 2022/23 baada ya mapitio ya mnyororo wa ugavi na mapendekezo ya maboresho ya usambazaji bidhaa za afya, umepelekea kuimarika kwa upatikanaji wa bidhaa hizo nchini.
Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa MSD, Hassan Ally Ibrahim ameyasema hayo leo katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO uliopo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maboresho ya mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya ikiwa ni mwendelezo wa taasisi kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Ibrahim amesema kuwa, hadi kufikia mwezi Juni 2023, MSD ilikuwa na mikataba ya muda mrefu 238 yenye jumla ya bidhaa za afya 2,004 ukiwa ni mkakati maalumu wa kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya ambapo katika kuendana na kasi ya ongezeko la vituo vya afya inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, MSD imekuwa ikifanya mawasiliano na balozi za Tanzania zilizopo China, Algeria, Korea ya Kusini, Urusi na maeneo mengine duniani ili kuweza kufanya utambuzi wa wazalishaji, wawekezaji na kuwezesha ununuzi wa bidhaa za afya kwa uhakika, ubora na gharama nafuu.
“Serikali kupitia MSD ilianza rasmi kutekeleza jukumu la usambazaji wa bidhaa za afya mara sita badala ya mara nne kwa mwaka kwa vituo vyote vya umma vya kutolea huduma za afya kwa mwaka wa fedha 2022/23. Usambazaji huu unaondoa tatizo la upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuhakikisha kwamba vituo vyote vinapelekewa bidhaa za afya hadi mlangoni mwa vituo vya kutolea huduma za afya kila baada ya miezi miwili,” amesema Meneja Ibrahim.
Katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali kupitia Bohari ya Dawa ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 157.56 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya za vituo vya kutolea huduma za afya ambapo kiasi hicho cha shilingi bilioni 157.56 ni kiasi cha juu kuwahi kutolewa na Serikali kupitia Bohari ya Dawa tokea kuanzishwa kwake miaka 30 iliyopita. Kiasi hicho ni sehemu tu ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ununuzi wa bidhaa za afya.
- Log in to post comments