Kamati ya CCM Mkoa wa Njombe, Yatembelea Kiwanda cha MSD- Idofi
NJOMBE
Kamati ya CCM Mkoa wa Njombe ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe.Deo Sanga, Mbunge wa jimbo la Makambako, imetembelea na kukagua maendeleo ya Mradi wa Kiwanda cha mipira ya mikono, kilichoko Idofi Makambako.
Kamati hiyo iliyoongozana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka imeelezea kufurahishwa na hatua zilifikiwa katika ujenzi wa mradi huo na kuipongeza Menejimenti na Wataalamu wa MSD kwa kufanikisha ujenzi huo.
Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Mhe. Deo Sanga, ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha nyingi kwaajili ya ujenzi huo, kwani utasaidia taifa katika upatikanaji wa bidhaa za afya na kuokoa matumizi ya fedha za kigeni.
Mhe.Deo Sanga ameiomba serikali sikivu ya Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, kumalizia angwe ya ujezi iliyobakia, ambayo inakadiriwa kugharimu takribani Bilioni 5 ili kukamilisha mradi huo.
Aidha Mhe. Deo Sanga amewaasa wakazi wa Idofi kulinda mradi huo, sambamba na kutumia fursa za uwepo wa mradi huo kujiinua kiuchumi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe amepongeza uwepo wa kiwanda hicho Idofi Makambako na kueleza kuwa mradi huo ni fahari kwa wana Njombe na Taifa kwa ujumla.
Kufuatia kiwanda hicho kuwa kwenye majaribio ya uzalishaji, wajumbe hao walipata sampuli za glavu za majaribio kwa ajili ya kuziweka ofisini kwao kama alama ya bidhaa inayozalishwa Mkoani kwao.
- Log in to post comments