Skip to main content
Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu Akiongea na Vyombo vya Habari Wakati wa Uzinduzi wa Usambazaji wa Vifaa vya Kuboresha Huduma za Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto

Waziri Ummy Azindua Usambazaji wa Vifaa Tiba vya Huduma za Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto

Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu azindua usambazaji wa vifaa vya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto vya zaidi ya sh.bilioni 14.9 ambavyo vitasambazwa katika majimbo 214 na halmashauri nchi nzima.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Makao Makuu ya Bohari ya Dawa (MSD) wakati wa uzinduzi huo, Waziri Ummy alisema uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya hivyo umelenga kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto na kuimarisha uzazi salama nchini.

Alisema lengo la Rais Dk.Samia ni kuokoa  maisha ya mama na mtoto hivyo vifaa vya zaidi ya sh. bilioni 14.9 ,  vitasambazwa katika majimbo 214 na halmashauri nchi nzima.

Waziri Ummy alitaja vifaa vilivyonunuliwa ambavyo vitasambazwa na MSD kuwa ni vitanda vya wagonjwa 3080, vitanda vya kujifungilia 1000, magodoro 5,500 mashuka 36808, meza za vitanda (overbed table) 306, ambapo vitasambazwa nchi nzima.

Alisema jitihada za serikali ya Rais Dk. Samia imefanikisha vifo vitokanavyo na uzazi kushuka  kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000.

“Pia vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimeshuka kutoka 67 kati ya vizazi hai 1000 mwaka 2015/16 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1000. Hii ni sawa na kupunguza vifo vya kinamama wajawazito kutoka 11,000 hadi vifo 2,500 kwa mwaka.

“Serikali itahakikisha nchi inafikia malengo ya kitaifa na kimataifa kama vile malengo endelevu ya Milenia 2030 yanayotutaka kupunguza athari za vifo vitokanavyo na uzazi hadi kufikia vifo chini ya 70 katika kila vizazi 100,000 vifo vya Watoto chini ya 38 katika kila vizazi hai 1,000 pamoja na vya Watoto chini 12 katika vizazi hai 1,000.”alisema.

Alisema Rais Dk. Samia anaguswa na vifo vya uzazi hivyo uwekezaji katika afya ya mama na mtoto unaendelea kwa kasi kwa kujenga vituo vya huduma za upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC) kutoka vituo 340 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 523 mwaka 2023.

Waziri Ummy alisisitiza kuwa, maboresho ya upatikanaji huduma hizo katika vituo vya kutolea huduma za afya yamesogeza huduma hizo za upasuaji karibu na wananchi kwa zaidi ya asilimia 75 hadi 85 na watu kupata huduma za afya  ndani ya Kilometa 5 ndani ya maeneo wanayoishi.

“Hali kadhalika Serikali imeendelea kuwekeza katika huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa kujenga wodi za uangalizi maalumu (NCU za watoto wachanga) zinazohudumia watoto wachanga walio mahututi kwa mara mbili zaidi kutoka 99 mwaka 2021 hadi 189 mwaka 2023,”alisema.

Waziri Ummy aliongeza kuwa, sambamba na kuboresha huduma hizo Serikali imeendelea kununua na kusambaza vifaa tiba na dawa na kuongeza wigo wa upatikanaji bidhaa za afya ya uzazi kutoka asilimia 82.5 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 88.2 mwaka 2023.

Pia kuajiri na kupeleka watumishi wenye sifa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchi nzima, kuajiri watumishi wa afya wapatao 28,759 hadi kufikia mwaka 2023.

Alisema kwa upande wa vitanda vua kutolea huduma za afya ya uzazi vimeongezeka kutoka vitanda 84,162 (mwaka 2021) hadi vitanda 104,687 (mwaka 2023).

Aidha wizara inategemea kupokea vifaa tiba vingine hivi karibuni ambavyo ni vitanda vya kujifungulia (4280), vitanda vya kufanyia uchunguzi (examination table) 4280, mkoba wa vifaa vya kujifungulia (delivery kit) 4280, kabati za vitanda(bed side lockers) 6420 na stendi ya dripu (6420).

Alisema katika kila jimbo litapata kila jimbo litapata vitanda  30, magodoro 30,  mashuka 60, makabati ya wodini 30, stendi za maji tiba 30, meza za kulia chakula 15 za wagonjwa, vitanda vya kujifungulia 10, seti ya vifaa tiba vya kujifungulia 10 na vitanda vya uchunguzi vya wodi ya wazazi 10

About MSD

Medical Stores Department (MSD) was established by the Act of Parliament No.13 of 1993 as an autonomous department under the Ministry of Health, Community Development, Gender, Elderly and Children responsible for developing, maintaining and managing an efficient and cost effective system of procurement, storage and distribution of approved medicines and medical supplies required for use by all public health facilities.