MSD yapokea vifaa tiba vya bil 10 kutoka kwa kampuni za Coca-Cola, Pepsi na Azam

Serikali imepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh bilioni 10 kutoka kwa umoja wa kampuni za utengenezaji wa vinywaji baridi nchini. Akipokea msaada huo kwa niaba ya Serikali Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alisema kuwa msaada huo ni mkubwa na wa aina yake na umekuja wakati muafaka wakati serikali ipo katika jitihada za kuboresha huduma za afya nchini.

Pia Majaliwa alisema anaimani kubwa na utendaji wa Bohari ya Dawa (MSD) chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu wake Bw. Laurean Bwanakunu, hivyo vifaa hivyo vitasambazwa kwa wakati uliopangwa, sehemu husika na kwa umakini mkubwa.

Majaliwa alisema kitendo cha kampuni hizo kutoa msaada huo mkubwa, ambao ameupokea ikiwa ni kontena 20 za futi 40 zenye makasha 1,500 ya vifaa vipya na vifaa mbalimbali zaidi ya 300 vikiwemo vitanda 80 na magodoro yake, unastahili kupongezwa na kila Mtanzania na kuungwa mkono na wadau wengine katika kunusuru afya za watanzania.

Mbali na msaada huo, lakini kampuni hizo kupitia Kampuni ya Coca-Cola italeta wataalamu kutoa mafunzo kwa watumiaji wa vifaa hivyo.

 

 

 

 

MSD yakabidhi vifaa vya mil 80.4 Hospitali ya Muhimbili

Bohari ya Dawa (MSD) hii leo tarehe 15/2/2016 imemkabidhi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi Mil. 80.4 kwa ajili ya wodi mpya ya wazazi iliyopo Muhimbili, vifaa hivyo ni pamoja na magodoro 120, mashuka 480 na vitanda 10 kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti). Vifaa hivi vimenunuliwa na Ofisi ya Rais Ikulu kwa ajili ya kuongeza idadi ya vitanda kukidhi mahitaji ya akina mama wanaojifungua na kulazwa katika wodi hiyo.

Akikabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bw. Laurean R. Bwanakunu amesema MSD imejitahidi kutekeleza kwa wakati agizo la Rais la kupeleka vifaa hivi kwenye Hospitali ya Muhimbili (Wodi mpya) katika jengo lililokuwa Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto.

Tayari MSD imeshavifikisha vifaa vyote Muhimbili vikisubiri kuingizwa katika jengo hilo.

 

 

Waziri wa Afya azindua duka la dawa la MSD Mwanza

 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amezindua rasmi duka la Dawa la MSD mkoani Mwanza ambalo liko ndani ya Hospitali ya Sekou Toure, na kufanya maduka ya MSD yaliyofunguliwa ndani ya maduka baada ya agizo la rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli kufikia mawili baada ya lile la Muhimbili lilifunguliwa mwaka jana mwishoni.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa duka hilo, ameipongeza MSD kwa hatua hiyo nzuri ya kufungua maduka ili kuwawezesha wananchi kupata dawa, na kuitaka MSD kukamilisha ufunguzi wa maduka mengine mawili yaliyosalia katika mikoa ya Arusha na Mbeya, kwani hicho ni moja ya kipaumbele katika uongozi wa serikali ya awamu ya Tano. Waziri huyo ameeleza kuwa Wizara yake imejiwekea malengo ya upatikanaji wa dawa nchini kutoka asilimia 70 kwa sasa kufika hadi asilimia 95.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bwana Laurean Bwanakunu amesema maduka mawili ya Arusha na Mbeya yamemekamilika, na yanatarajia kufunguliwa hivi karibuni, na kwamba kwa mikoa mingine wameshafanya mawasiliano na kwamba tayari MSD imefanya mazungumzo na viongozi wa mikoa Ruvuma, Rukwa, Singida, Dodoma, Geita, Kagera na Iringa kufungua maduka yao ya dawa ambapo MSD itawauzia dawa. “Tutakachofanya, sisi (MSD) tutawapa utaalamu na kuwawezesha utaalam wa uendeshaji maduka hayo” alieleza Bwanakunu.

 

 

 

 

Naibu Waziri wa Afya azindua duka la dawa la MSD Arusha

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt Hamis Kigwangalla amezindua rasmi duka la Dawa la MSD jijini Arusha, ambalo liko ndani hospitali ya Mount Meru na kuiagiza MSD mbali na kuweka alama ya GoT kwenye vidonge vyake iangalie pia utaratibu wa kuweka rangi maalumu kwenye vidonge na vifungashio, ili kurahisha udhibiti wa upotevu na ufuatiliaji wa dawa hizo. Naibu Waziri huyo pia amewahimiza watendaji wa MSD kuwa waadilifu, kuwajali na kuwasilikiza wateja na kutumia lugha nzuri wakati wa kuwahudumia wateja, huku akitoa angalizo kwa wale wanaokiuka taratibu za ajira kuwa watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD Prof. Idris Mtulia ameeleza kuwa MSD inaweza kufanya vizuri zaidi endapo changamoto za sheria ya manunuzi, mgawo mdogo wa fedha kwa vituo vya Afya, hospitali na zahanati, na mgawo wa fedha kuja kwa mafungu zitafanyiwa kazi. Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bwana Laurean Bwanakunu ameeleza kuwa MSD itakuwa na maduka manne tu mkoani Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya ambapo kwa mikoa mingine MSD itafanya mawasiliano na hospitali za mikoa ziwe na maduka ya hospitali wanayoendesha wenyewe na kasha MSD iwauzie dawa na kuwawezesha utaalamu wa kuendesha maduka hayo.

 

 

 

Waziri wa Afya afanya ziara MSD

Waziri wa Afya , Maendeleoya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametembelea Makao Makuu ya Bohari ya Dawa (MSD) na kuahidi kuwa balozi wa kuhakikisha deni la serikali linalipwa ili kuiwezesha MSD kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Waziri huyo ameeleza hayo baada ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bwana Laurean Bwanakunu kueleza kuwa ukosefu wa fedha na deni la serikali ni changamoto kubwa inayoathiri utekelezaji mzuri wa majukumu ya MSD.

Mbali na hilo, waziri huyo wa Afya amesema mbali na deni hilo, hata kiasi cha fedha kinachotengwa na serikali kwaajili ya Hospitali, vituo vya Afya na zahanati kununua dawa hakitoshelezi mahitaji, hivyo lazima suala hilo lifanyiwe kazi mapema, huku akisistiza hata kiasi hicho kidogo kinachopatikana kitumike vizuri.

Katika hatua nyingine ameishauri Bohari ya Dawa kuanza utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, kuhakikisha dawa muhimu zinapatikana wakati wote na kuiagiza MSD itangaze kwenye vyombo vya habari dawa zote ambazo zinapelekwa vituoni, zahanati na kwenye hospitali, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bwana Laurean Bwanakunu ameeleza kuwa tayari MSD imeshaanza kubandika kwenye mbao za matangazo za hospitali orodha ya dawa inazofikisha.

Waziri huyo ambaye alifuatana na Katibu Mkuu wa Wizara yake na watendaji wengine alitembelea maghala ya kuhifadhia dawa ya Makao Makuu, jingo la ofisi linalojengwa pamoja na kuwa na mkutano na menejimenti ya MSD, ambapo pamoja na mambo mengine ameipongeza MSD kwa hatua iliyofikia ya kuweka nembo ya GOT kwenye vidonge vyake ili kudhibiti upotevu wa dawa za serikali pamoja na kuanzisha maduka ya dawa Muhimbili, na mengine yanayotarajia kufunguliwa hivi karibuni mkoani Mbeya, Arusha na Mwanza.

Waziri Ummy Mwalimu alihitimisha kwa kusema kuwa ajenda yake kuu ni upatikanaji wa dawa kwa wakati, kama rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Magufuli alivyoaainisha, hivyo MSD itekeleze majukumu yake ipasavyo kwani mafanikio ya MSD ni mafanikio kwake pia.

 

Lock full review www.8betting.co.uk 888 Bookmaker