Mawaziri wa Afya wa SADC Waitembelea MSD
(Mawaziri wa Afya kutoka nchi za SADC wakimakinikia mada, mara walipotembelea MSD)
Mawaziri kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC) wanaoshughulikia masuala ya Afya na Ukimwi wametembelea Ofisi za Bohari ya Dawa (MSD) zilizoko Keko, jijini Dar es Salaam nakushuhudia jinsi mnyororo mzima wa ugavi unavyofanya kazi.
Mawaziri hao wameonyesha kuridhishwa na kufurahishwa na jinsi MSD ilivyojipanga katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,mathalani ununuzi, uhifadhi, na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara huku wakibainishakuwa ni mfano wa kuigwa kwa nchi wanachama. (Mawaziri wa Afya kutoka nchi za SADC wakimakinikia mada, mara walipotembelea Bohari ya Dawa (MSD))
Mawaziri hao wanaoshughulika na afya wameambatana na mwenyeji wao Waziri wa afya wa Tanzania, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb), ambaye amewaeleza waandishi wa habari utayari wa MSD katika katika kufanya manunuzi ya pamoja kwa nchi za SADC na mchakato mzima uliopelekea MSD kupewa zabuni hiyo.
Aidha, amebainisha kuwa lengo la ziara hiyo ya Mawaziri ni kuangalia uwezo, vifaa na utaalamu wa MSD katika kutekeleza majukumu hayo kwa nchi wanachama.
(Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bw. Laurean Bwanakunu, akitoa mada)
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bw. Laurean Bwanakunu, ametoa tathimini ya ulipofikia mchakato mzima wa manunuzi ya pamoja, kwa nchi wanachama hadi sasa (SPPS), ambapo amebainisha kwamba wamekwisha pata wazabuni na sasa mikataba iko kwa Mwanasheria Mkuu ikifanyiwa upembuzi, (Vetting).
Aidha amewahakikishia mawaziri hao kutoka SADC kuwa mchakato wa manunuzi ya pamoja utapunguza gharama kwa kiasi kikubwa kwa nchi wanachama na kukuza uchumi wa viwanda kupitia uwekezaji wa viwanda vya dawa.
Mawaziri hao kutoka SADC, walipata fursa ya kutembelea magahala ya kuhifadhia dawa ya MSD na kujionea jinsi kazi mbalimbali za utunzaji na ugavi, zinavyofanyika kwa weledi na ufanisi mkubwa.
|