Mkurugenzi Mkuu NHIF Aipongeza MSD
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga, ameipongeza MSD kwa kuboresha mfumo wake wa manunuzi ya vifaa vya maabara na vitendanishi vyake, kwa kwenda kununua vifaa hivyo moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji. Ameongeza kuwa hatua hiyo itarahisha upatikanaji wa vifaa hivyo nchini na kupunguza gharama za huduma za vipimo vya kimaabara kwa wananchi.
Bw. Konga ametoa pongezi hizo alipotembelea Makao Makuu ya MSD kwa lengo la kuboresha uhusiano na ushirikiano wa kikazi baina ya MSD na NHIF, mathalani katika kuboresha huduma za kimaabara kwenye vituo vya kutolea huduma za afya chini.
Kwa upande wake Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa MSD Bw. Joseph Kitukulu, amesema gharama za vifaa hivyo na vitendanishi zimepungua kwa zaidi ya asilimi 50, ambapo vituo vya kutolea huduma za afya vya ngazi zote nchini wanaweza kuwa navyo.
Aliongeza kuwa vifaa hivyo ni pamoja na mashine ya kupima wingi wa damu, sukari na zile za kupima kiwango cha kemikali mwilini. Aidha kwa upande wa mashine za kuchuja damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo, mashine zilizonunuliwa zitawezesha kushuka kwa gharama za uchujaji wa damu kwa wagonjwa hao kwa kiasi kikubwa. Tayari vituo vya afya nchini vimeanza kununua mashine hizo kutoka MSD, huku wataalamu wa maabara wa MSD wakiendelea kukutana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuzitambulisha mashine hizo na kujiridhisha kuhusu utendaji kazi wake.
|