Waziri wa Afya azindua duka la dawa la MSD Mwanza
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amezindua rasmi duka la Dawa la MSD mkoani Mwanza ambalo liko ndani ya Hospitali ya Sekou Toure, na kufanya maduka ya MSD yaliyofunguliwa ndani ya maduka baada ya agizo la rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli kufikia mawili baada ya lile la Muhimbili lilifunguliwa mwaka jana mwishoni.
Katika hotuba yake ya uzinduzi wa duka hilo, ameipongeza MSD kwa hatua hiyo nzuri ya kufungua maduka ili kuwawezesha wananchi kupata dawa, na kuitaka MSD kukamilisha ufunguzi wa maduka mengine mawili yaliyosalia katika mikoa ya Arusha na Mbeya, kwani hicho ni moja ya kipaumbele katika uongozi wa serikali ya awamu ya Tano. Waziri huyo ameeleza kuwa Wizara yake imejiwekea malengo ya upatikanaji wa dawa nchini kutoka asilimia 70 kwa sasa kufika hadi asilimia 95.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bwana Laurean Bwanakunu amesema maduka mawili ya Arusha na Mbeya yamemekamilika, na yanatarajia kufunguliwa hivi karibuni, na kwamba kwa mikoa mingine wameshafanya mawasiliano na kwamba tayari MSD imefanya mazungumzo na viongozi wa mikoa Ruvuma, Rukwa, Singida, Dodoma, Geita, Kagera na Iringa kufungua maduka yao ya dawa ambapo MSD itawauzia dawa. “Tutakachofanya, sisi (MSD) tutawapa utaalamu na kuwawezesha utaalam wa uendeshaji maduka hayo” alieleza Bwanakunu.