MSD NA WADAU WA AFYA WAASWA KUZINGATIA WAJIBU KATIKA JAMII
Mwanza. Wadau wa afya Mkoa wa Mara pamoja na Bohari ya Dawa (MSD) wametakiwa kuzingatia wajibu wao katika jamii, kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kutoa huduma bora za afya, ili kuunga mkono kwa vitendo, juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuboresha huduma za afya nchini.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Bw. Masarika Robert Makungu, wakati akifungua kikao kazi baina ya MSD Kanda ya Mwanza na Wadau wake kilichofanyika jijini Mwanza kwa lengo la kujadili namna ya kuboresha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.
Bw. Makungu ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya afya, kwa lengo la kuboresha afya za wananchi na kuongeza nguvu kazi ya taifa, hivyo ni lazima kuwe na matokeo chanya na yenye tija kupitia watendaji.
"Kikao hiki kitatoa nafasi kwa watendaji kuchakata, kujadili na kupata suluhu ya ukosefu wa baadhi bidhaa za afya, hasa vifaa tiba na mwisho kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuhakikisha tija kubwa inaonekana katika uwekezaji mkubwa ambao serikali ya Awamu ya Sita imefanya". Alisema Bw. Makungu.
Sambamba na hilo ameipongeza MSD kwa maboresho mbalimbali ambayo imekua ikiyafanya ikiwemo kupunguza muda wa kusubiri bidhaa. Hata hivyo, Bw. Makungu amewataka wadau hao wa afya Mkoani humo kufanya maoteo sahihi ya bidhaa za afya ili kuipa ahueni MSD katika kuihudumia jamii.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu amesema wamejipanga kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya unaimarika, hivo kikao hicho kimekuja wakati muafaka, kwani serikali imewekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya afya Mkoani humo.
Aidha amepongeza MSD kwa kurudisha vikao vya wadau ili kuwekana sawa, huku akiahidi kusimamia kikamilifu masuala mbalimbali, ikiwemo maoteo suala ambalo limeonekana ni changamoto kupitia kikao hicho.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Mwanza, Bw. Egidius Rwezaura amewashukuru wajumbe hao kwa muitikio wao, huku akibainisha maboresho mbalimbali yanayofanywa na MSD kwa sasa ikiwemo maboresho ya mfumo wa usambazaji, mikataba ya muda mrefu kwa wazalishaji na washitiri, uanzishaji wa viwanda vya bidhaa za afya, maboresho ya huduma, sambamba na rasilimali watu. |