Kamati ya CCM Mkoa wa Njombe, Yatembelea Kiwanda cha MSD- Idofi

WhatsApp_Image_2023-02-06_at_15.10.15.jpeg

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe Mhe. Deo Sanga, Akiongea na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Antony Mtaka Pamoja wa Wananchi Wengine, Wakati Kamati ya CCM Mkoani Humo ilipotembelea Kiwanda cha Mipira ya Mikono cha MSD- Idofi, Kilichoko Makambako, Mkoani Njombe.

 

 

NJOMBE

Kamati ya CCM Mkoa wa Njombe ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe.Deo Sanga, Mbunge wa jimbo la Makambako, imetembelea na kukagua maendeleo ya Mradi wa Kiwanda cha mipira ya mikono, kilichoko Idofi Makambako.

 

Kamati hiyo iliyoongozana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka imeelezea kufurahishwa na hatua zilifikiwa katika ujenzi wa mradi huo na kuipongeza Menejimenti na Wataalamu wa MSD kwa kufanikisha ujenzi huo.

 

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Mhe. Deo Sanga, ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha nyingi kwaajili ya ujenzi huo, kwani utasaidia taifa katika upatikanaji wa bidhaa za afya na kuokoa matumizi ya fedha za kigeni.

 

Mhe.Deo Sanga ameiomba serikali sikivu ya Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, kumalizia angwe ya ujezi iliyobakia, ambayo inakadiriwa kugharimu takribani Bilioni 5 ili kukamilisha mradi huo.

 

Aidha Mhe. Deo Sanga amewaasa wakazi wa Idofi kulinda mradi huo, sambamba na kutumia fursa za uwepo wa mradi huo kujiinua kiuchumi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe amepongeza uwepo wa kiwanda hicho Idofi Makambako na kueleza kuwa mradi huo ni fahari kwa wana Njombe na Taifa kwa ujumla.

 

Kufuatia kiwanda hicho kuwa kwenye majaribio ya uzalishaji, wajumbe hao walipata sampuli za glavu za majaribio kwa ajili ya kuziweka ofisini kwao kama alama ya bidhaa inayozalishwa Mkoani kwao

MSD Yafuatilia Ubora wa Dawa-Vituoni

WhatsApp_Image_2023-02-06_at_16.27.20.jpeg

 

 

Bohari ya dawa (MSD) kupitia Kitengo chake cha Udhibiti Ubora imeendelea na zoezi la ufuatiliaji wa ubora wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara ambavyo vimeshasambazwa kwa wateja ili kuhakikisha bidhaa hizo za afya hasa dawa, zinaendelea kuwa na ubora unaotakiwa.

 

Zoezi hili ni muongozo uliotolewa na Shirika la Afya duniani (WHO) pamoja na ushauri wa Mamlaka ya Dawa na vifaa tiba (TMDA) kuitaka MSD kama msambazaji wa bidhaa za afya nchini kufuatilia ubora wa bidhaa ambazo tayari zipo kwa wateja na kujionea jinsi zinavyotunzwa, ili kulinda afya za watumiaji kwani kumekuwepo na changamoto nyingi kwenye mnyororo wa ugavi wa dawa, zinazoweza kuathiri ubora wa awali wa dawa na vifaa tiba, ikiwemo namna ya usafirishaji, utunzaji na hali ya hewa kwenye maeneo yao.

 

Katika mwaka wa Fedha 2022/2023 tayari zoezi hili limeshafanyika katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Kilimanjaro na Tanga kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati, huku zoezi hilo likitarajiwa kuendelea kwenye mikoa mingine.

 

Zoezi hili hutekelezwa kila mwaka ili kulinda afya za watumiaji ikiwa ni pamoja na kushauri juu ya mapungufu yatakayoonekana katika vituo vya kutolea huduma za afya, ili kuepusha athari za ubora wa bidhaa hizo.

 

Zoezi hili huangazia namna ya usafirishaji, utunzaji na hali ya hewa kwenye maeneo ambapo bidhaa hizo huhifadhiwa katika vituo hivyo.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Atembelea Kiwanda cha MSD-Idofi

web-1.jpeg

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Antony Mtaka, Akipokea Maelezo kuhusu Uzalishaji wa Kiwanda cha Mipira ya Mikono cha MSD- Idofi, kutoka kwa Msimamizi Mkuu wa Mradi huo, Bi. Selwa Hamid.

 

 

 

NJOMBE

 

Mkuu wa mkoa wa Njombe Mhe. Antony Mtaka na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Njombe imetembelea kiwanda cha Bohari ya Dawa (MSD) cha kuzalisha mipira ya mikono kilichopo Idofi, Makambako ambacho ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 70.

Mhe.Mtaka amesema kiwanda hicho ni muhimu kwa sekta ya afya kwani kitapunguza matumizi ya fedha za kigeni kununua bidhaa hiyo nje ya nchi na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mipira ya mikono nchini.

Mtaka aliiagiza MSD ikamilishe kiwanda hicho ili uzalishaji uanze ili wananchi wanufaike na mradi huo na kutafuta masoko nchi za SADC.

Mwenyekiti wa bodi ya Wadhamini ya MSD Rosemary Silaa amesema kiwanda hicho kitatoa ajira 200 huku Mkurugenzi Mkuu MSD Mavere Tukai akieleza kuwa uzalishaji wa mipira ya mikono kiwandani hapo unatarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.

Uzalishaji wa kiwanda hicho utaiwezesha MSD kukidhi mahitaji yake kwa asilimia 83.4 ya mahitaji ya mipira ya mikono nchini.

Kwa upande wake Mfamasia Mkuu wa Serikali Daudi Msasi amesema serikali kupitia Wizara ya Afya inaunga mkono uanzishwaji wa viwanda vya bidhaa za afya, na watahakikisha kiwanda hicho kinaanza uzalishaji.

Kiwanda hicho kitaokoa matumizi ya fedha za kigeni Bilioni 24 kwa mwaka ambazo zingenunua bidhaa hiyo nje ya nchi.

MSD Yaboresha Huduma za Kusafisha Damu-Tumbi

web_3.jpeg

Baadhi ya Vitanda na Mashine za Kisasa, Vikiwa Vimesimikwa Kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani- Tumbi, Kufuatia Maboresho ya Huduma ya Kuchuja Damu

 

PWANI

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani - Tumbi imeanza kutoa huduma mpya ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo. Huduma hii imeanza kutolewa baada ya Bohari ya dawa (MSD) kukamilisha kufunga  mashine za kisasa 10 za kusafisha damu baada ya kuboresha miundombinu ya kuwezesha huduma.

 

Hatua hiyo ni muendelezo wa maboresho ya huduma za afya nchini yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Afya.

 

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Amani Malima amesema mpaka sasa tayari huduma imeshatolewa kwa wagonjwa watatu na huduma hiyo imefanikiwa kwa asilimia100.

 

Kwa upande wake Fundi Sanifu vifaa tiba wa MSD Ikunda Harrison amesema mbali na kufunga mashine hizi MSD ilitoa mafunzo kwa watoa huduma wa hospitali hiyo, ambapo  kwa sasa jukumu kubwa la MSD ni kuhakikisha vitendanishi vya mashine hizo vinaendelea kuwepo wakati wote ili kuepuka kukwamisha huduma

MSD Yapokea Shehena ya Vipimo vya UKIMWI na Kaswende

MSD-2.jpeg

 

Vipimo vya UKIMWI na Kaswende Vikiwa Vimepokelewa Ghalani Tayari kwa Usambazaji

 

 

DAR-ES-SALAAM

 

Katika kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani MSD imeendelea kupokea na kusambaza bidhaa mbalimbali za afya za kupambana na kudhibiti maambukizi ya Virusi vya UKIMWI Pamoja na Kaswende.

 

Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai ameeleza kuwa miongoni mwa bidhaa za afya ambazo kwa sasa inauhitaji mkubwa na inaendelea kusambazwa na MSD kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ni vipimo vya kupima maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na gonjwa la zinaa la Kaswende (HIV/ Syphilis Duo).

 

Vipimo hivyo vinafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa kupambana UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria  (The Global Fund) na pia hutumika kupima akina mama wajawazito kutambua maambukizi ya magonjwa yote mawili kwa wakati mmoja.

 

Kwa mujibu wa Dr. Ibadi Kaondo wa MSD, vipimo hivyo vinamsaidia mama mjamzito kutambua hali ya afya mapema, na endapo maambukizi yamegundulika inarahisisha kuanza matibabu mapema ili kufubaza makali ya virusi vya ukimwi na kutibu kaswende kwa ajili kuimarisha afya ya mzazi na kumkinga mtoto dhidi ya Maambukizi ya VVU, Kaswende ama kujifungua mtoto mfu.

 

Hapo awali vipimo hivi kila kimoja kilikuwa kinajitegemea, ambapo vilitumia muda mrefu kutoa majibu.  MSD kwa sasa ina shehena ya kutosha ya vipimo hivyo ambavyo tayari baadhi vilishaanza kusambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

 

Maadhimisho ya kitaifa ya siku ya UKIMWI duniani kwa mwaka 2022, yamefanyika katika viwanja vya Ilulu Mkoani Lindi, yakihudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali huku mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Lock full review www.8betting.co.uk 888 Bookmaker