Katibu Mtendaji SADC Atembelea MSD
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Mpedi Magosi (watatu kushoto) na Wajumbe Alioambatana Nao, Wakiwa Kwenye Picha ya Pamoja na Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Bohari ya Dawa (MSD), Mara Baada ya Kutembelea Ofisi za Bohari hiyo, Zilizoko Keko, jijini Dar es Salaam
DAR ES SALAAM: Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Mpedi Magosi pamoja na ujumbe wake, wametembelea Makao Makuu ya Bohari ya Dawa (MSD), yaliyoko Keko jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujionea jinsi taasisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake sambamba na kupokea mrejesho wa maendeleo ya utekelezaji wa mpango wa manununzi ya pamoja (SPPS) kwaajili ya nchi wanachana.
Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti ya Bohari ya Dawa, Kaimu Mkurgenzi Mkuu wa Bohari hiyo Bw. Leopold Shayo amempongeza Katibu Mtendaji huyo wa SADC kwa kuzuru Tanzania, na hasa kuitembelea MSD, huku pia akianisha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika Jumuiya hiyo kupitia utekelezaji wa mpango wa manunuzi ya pamoja kwa nchi wananchama.
kwa nchi za SADC (SPPS) imewezesha kuundwa kwa Miongozo ya SPPS na Mfumo wa Usimamizi wa mnyororo wa Ugavi kwa nchi wanachama, kuitisha na kuendesha mkutano wa kitaalamu wa SADC Pooled Procurement wa kikanda ili kuwezesha kubadilishana taarifa.
Ameongeza kwamba hadi sasa MSD imeweza kutengeneza mfumo kielektroniki (e-SPPS) ili kusaidia kushughulikia miamala yote ya usimamizi wa ugavi wa SPPS ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, ambamba na kuwezesha kusainiwa kwa mikataba 41 na watengenezaji wa bidhaa za afya.
Aidha, Bw. Shayo amesisitiza kwamba MSD imewezesha kukuza uelewa juu ya matumizi ya mfummo wa SPPS kwa kufanya mikutano na Mabalozi wa SADC walioidhinishwa na Tanzania na nchi za SADC, ambapo hadi kufikia Februari 2022, nchi tatu (3) Wanachama zilikuwa zimeanza kutumia mfumo wa SPPS, ambazo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Comoro, na Seychelles huku zikiokoa kati ya 35% -70% ya gharama za unununzi wa bidhaa za afya.
Katika hatua nyingne nchi tatu (3) zaidi ambazo ni wanachama wa Jumuiya hiyo ambazo ni Msumbiji, Malawi na Botswana zimeonyesha nia na utayari wa kutumia jukwaa la SPPS, kutokana na mafanikio yaliyopatikana kupitia mfumo huo wa manunuzi ya pamoja.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Lojistiki wa MSD, Bw. William Singano, amesema mbali na mafanikio yaliyopatikana kupitia mfumo huo wa manunuzi ya pamoja, bado kuna uhitaji wa msukumo kwa nchi wanachama kutumia mfumo huo ili kuwezesha lengo mahususi la uanzishwaji wa ushirikiano huo kutimia.
Bw. Singano ameuomba uongozi huo wa SADC, kusaidia upatikanaji wa taarifa za kikanda za wazalishaji wa ndani, walioko ndani ya jumuiya, hatua itayosaidia kuwawezesha kushiriki katika manunuzi ya bidhaa za afya na kuongeza pato na ajira kwa nchi wanachama.
Aidha ameuomba uongozi huo wa SADC, kusaidia upatikanaji wa watu mahususi (conctact person) kutoka nchi wanachama watakao kuwa wakisimamia mfumo na taarifa zinazohusiana na SPPS. Sambamba na hilo ameuomba uongozi huo kusaidia upatikanaji wa orodha mahsusi ya bidhaa muhimu za afya 83, pamoja na wazalishaji ili kusiaidia katika mipango ya manunuzi na uzalishaji.
Kwa upande wake Katibu wa SADC Mhe. Elias Mpedi Magosi ameeleza kuwa Tanzania kuwa mnunuzi mkuu wa dawa kwa nchi za Ukanda wa SADC ni heshima kubwa kwa Taifa, kuaminiwa kwa huduma bora, uwezo na kukidhi vigezo vya kitaalamu katika mnyororo wa ugavi.
Ameupongeza uongozi wa MSD kwa hatua kubwa uliopiga katika mpango wa manunuzi ya pamoja, huku akiahidi kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na MSD, ili kuleta tija na msukumo wa manunuzi ya pamoja ya bidhaa za afya kwa nchi wanachama.
Hatahivyo; ameitaka MSD kuongeza nguvu na ubunifu ili kuvutia nchi nyingi zaidi na kuhakikisha kwamba lengo linafikiwa, huku akipongeza mpango wa kutoa kipaumbele kwa wazalishaji wa ndani, kwani utainua uchumi wa nchi wanachama pamoja na kuongeza ajira. |