Serikali Kuendelea Kuunga Mkono, Ujenzi wa Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba vya MSD.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu Akiongea Mbele ya Wananchi wa Mji wa Mkambako (Hawapo pichani) Juu ya Hatua Ujenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaa Tiba, Wakati wa Ziara ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan Mkoani Njombe
NJOMBE: Serikali imeahidi kuendelea na ujenzi wa Kiwanda cha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba kilichopo chini ya Bohari ya Dawa (MSD), huko Idofi Makambako, Mkoani Njombe, ilikuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini sambamba na kuokoa matumizi ya fedha za kigeni.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo, alipokua akitoa salamu zake kwa wananchi wa Makambako mara baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza kwenye ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa Makambako - Njombe.
"Mheshimiwa Rais, hapa Makambako tunajenga kiwanda cha Dawa na Vifaa tiba ambapo ujenzi wake hapo nyuma ulisimama kwakuwa tunarekebisha mambo kadhaa, lakini sasa tunaendelea na ujenzi" amesema Waziri Ummy Mwalimu.
"Nimesimama hapa kuwahakikishia wana Makambako, serikali itaendeleza na kukamilisha ujenzi wa kiwanda hiki, na tutaleta shilingi Billioni 17 kukamilisha ujenzi" Alisisitiza Mhe. Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema hadi sasa serikali imekwisha toa kiasi cha shilingi Bilioni 18 ikiwa ni kwa ajili ya ujenzi pamoja na kununua baadhi ya mashine na hadi kukamilika kwake, kiwanda hicho kitagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 35.
Aidha Waziri Ummy ameongeza kwamba, kiwanda hicho kitazalisha dawa za vidonge, (tablets), dawa za maji (syrup), pamoja na mipira ya mikono (gloves), huku kikitarajia kutoa ajira kwa watu zaidi ya 200. |