Makamu wa Rais Aipigia Chapuo MSD Kusambaza Dawa SADC
,
Makamu wa Rais ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 7, 2019 wakati akifungua Mkutano wa mawaziri wanaoshughulikia sekta ya afya na UKIMWI kutokanchi 16 wanachama uliomalizika leo, jijini Dar es Salaam.
Amesisitiza kuwa MSD kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mchakato huo, kwa kusaini mikataba na wazalishaji baada ya kutangaza zabuni.
“Ninapenda kuwadhibitishia kwamba MSD imejipanga vizuri kuhakikisha jukumu hili la uratibu wa manunuzi ya pamoja linatekelezwa kwa ufanisi na kwamba hivi sasa taasisi hiyo inaendelea na kusaini mikataba na wazalishaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi,” alisema Samia
Ameongeza kuwa Serikali imejenga kiwanda cha kutengeneza dawa ya viuadudu chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 6 kwa mwaka na kwamba dawa zinazozalishwa zinatumika kudhibiti wadudu dhurifu wakiwemo viluwiluwi vya mbu wanaosababisha malaria.
“Nitumie fursa hii kuhamasisha nchi za SADC zinunue dawa ya viuadudu inayozalishwa na kiwanda hiki kilichoko nchini kupitia utaratibu wa manunuzi ya pamoja wa nchi za SADC unaoratibiwa na Bohari ya Dawa MSD,” amesema.
Novemba mwaka 2017 Tanzania kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ilishinda zabuni ya usambazaji wa dawa kwa nchi za SADC jukumu ambalo ilipewa na mkutano wa mawaziri wa afya na UKIMWI kutoka nchi wanachama.
Mchakato wa kusaini mikataba unaenda sambamba na kutoa mafunzo kwa watendaji kutoka nchi wanachama juu ya namna ya kutumia mfumo wa kielektroniki wa uagizaji wa dawa, ambao MSD unautumia katika uagizaji, ununuzi na usambazaji.
Aidha mawaziri hao watapata fursa kuitembelea MSD siku ya kesho Ijumaa Tarehe 7, 11, 2019 ili kujionea utendaji wake.
|