Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Yaipongeza MSD kwa Kupata Hati Safi ya Ukaguzi wa Hesabu Zake
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe.Naghenjwa Kaboyoka ameipongeza MSD kwa kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu zake, na kuitaka kuendeleza rekodi hiyo safi kwa ustawi wa taasisi hiyo kiutendaji. Ametoa pongezi hizo leo Kamati hiyo ilipokuwa ziarani MSD, ambapo ilipokea taarifa ya utendaji ambayo inafafanua mikakati ya maboresho ya utendaji wa MSD, mwenendo wa mapato na matumizi ya fedha na Mnyororo wa Ugavi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara. Ameipongeza pia MSD kwa kuteuliwa kuwa mnunuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kusema kuwa hiyo ni heshima kubwa kwa Taifa.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD Dkt. Fatma Mrisho ameihakikishia Kamati hiyo kuwa, pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili MSD bado inaendelea kutoa huduma bora na za kiwango cha juu kwa wananchi na kusimamia mnyororo wa ugavi ili kuleta tija kwenye mfumo wa afya wa nchi. Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bw. Laurean R. Bwanakunu amesema MSD inajipanga sasa kuhakikisha inafanyia kazi maoni na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na kamati hiyo kwani ni maelekezo yenye lengo la kuiboresha MSD, ili izidi kutimiza majukumu yake ya kila siku kwa ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
|