MSD yapiga hatua kuwezesha uzalishaji dawa kwa njia ya ubia na sekta binafsi) PPP
Bohari ya Dawa (MSD) pamoja na Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa pamoja leo wamesaini makubaliano ya umilikishwaji wa eneo la ardhi, lenye ukubwa wa mita za mraba 400,000 ambayo itatumika kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha kuzalishia dawa na vifaa tiba.
Hatua hiyo ni Utekelezaji wa mradi wa uzalishaji dawa kwa ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi yaani PPP, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bwana Laurean Bwanakunu amesema dhamira ya serikali ya viwanda inawezesha mambo makubwa mawili ambayo ni upatikanaji wa ardhi na kisha kutafuta wawekezaji ama soko.
Amesema baada ya hatua hii watatangaza zabuni kwa ajili ya kupata wazalishaji wa dawa na vifaa tiba kama vile maji ya dripu, pamba,gozi na dawa za maji za watoto ambayo itasaidia kupunguza gharama za kuagiza dawa kutoka nje ya nchi, ambapo 85% ya dawa na vifaa tiba vinaagizwa kutoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Bi. Jenifa Omolo eneo hilo lipo karibu na miundombinu ya reli na barabara hivyo itakuwa ni hatua ya kuleta maendeleo kwa mji wa Kibaha.
====