Upatikanaji wa dawa waimarika MSD kutoka 54% iliyokuwepo mwaka jana, hadi kufikia 74% hivi sasa

Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurean Bwanakunu amesema hali ya upatikanaji wa dawa kwa sasa imeboreshwa kutoka asilimia 54 iliyokuwepo mwaka jana, hadi kufikia asilimia 74 hivi sasa. Ameuhakikishia umma kuwa upatikanaji wa dawa utaimarika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu hadi kufikia asilimia 90.

Amesema kwa sasa kati ya aina za dawa muhimu 135 zinazohitajika kuwepo MSD dawa aina 100 zinapatika kwenye maghala ya MSD

Mkurugenzi wa MSD, Bwanakunu ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari, Idara ya habaari Maelezo, alipokuwa kwenye mkutano ulioandaliwa na idara katika jukumu lake la kutoa nafasi kwa Idara na Taasisi za serikali kuelezea utekelezaji wa majukumu yao.

Katika hatua nyingine, Bwanakunu ameeleza kuwa, MSD imefanikiwa kurejesha maghala iliyokuwa imekodi kwa ajili ya kuhifadhia vifaa tiba, hatua ambayo inaokoa shilingi Bilioni 4 ambazo zilikuwa zikilipwa kama kodi kila mwaka. Ameongeza kuwa, tayari wamekabidhiwa kiwanja eneo la Luguruni, wilayani Ubungo walichopewa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli ambacho kitatumika kujenga ofisi za Kanda ya Dar es Salaam.

Kuhusu maduka, ameeleza kuwa wiki ijayo wanatarajia kuzindua duka la dawa la MSD mkoani Katavi, ambalo litaifanya MSD kuwa na jumla ya maduka Saba, mengine yakiwa mkoani Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Lindi, Geita na Mbeya.

Akijibu swali juu ya ukosefu wa vifaa vya kujifungulia akina mama Mkurugenzi Mkuu amesema vipo vya kutosha, na zabuni ya manunuzi ya vifungashio kwa ajili ya vifaa hivyo vya kujifungulia iko katika mchakato wa kumpata mshitiri. Ameeleza kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu anaangalia namna ya kuwawezesha akina mama wasiokuwa na uwezo wa kununua vifaa hivyo. Utaratibu huo atautoa baadae.

Kwa sasa MSD inanunua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba unakuwa endelevu na kupunguza gharama za ununuzi wa dawa hizo, ambazo asilimia 80 zinatoka nje ya nchi.

Lock full review www.8betting.co.uk 888 Bookmaker