Dkt. Mollel Apongeza Maboresho ya Huduma za MSD

MTWARA-1.jpgNaibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel, Akiwa na Viongozi Wengine wa Wizara, Wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai, Mara Baada ya Viongozi Hao Kutembelea Eneo la Mikindani Mkoani Mtwara, Linapojengwa Ghala Jipya la MSD, Mkabala na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini

MTWARA.

NAIBU Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema ameridhishwa na mabadiliko yanayofanywa na Bohari ya Dawa (MSD) hususani katika utendaji na utekelezaji wa mikataba ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

 

Dk. Mollel amesema hayo jana mkoani Mtwara katika ziara ya kikazi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. John Jingu walipotembelea ofisi za Bohari ya Dawa Kanda ya Mtwara, kujionea hali ya utoaji wa huduma na changamoto ya ufinyu wa ghala unaoikabili kanda hiyo.

 

Akizungumza na watumishi wa Kanda hiyo, Dk. Mollel amesema, ameridhishwa na mabadiliko yanayofanywa na MSD hususani katika utendaji na utekelezaji wa mikakati ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

 

Aliongeza kuwa hatua ya Serikali kuazimia kuipatia MSD mtaji ni ya kujivunia, kwani itasaidia kuhakikisha MSD inatekeleza mipango mikakati yake, ikiwemo ujenzi wa maghala na kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana nchini kote.

 

Sambaba na kutemebelea ofisi za Kanda hiyo, Uongozi huo pia ulizuru eneo la Mikindani Mkoani Mtwara, ambalo lipo mkabala na hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini, mahali linapojengwa ghala jipya la Bohari ya Dawa Kanda ya Mtwara na kujionea jinsi mchakato wa ujenzi wa ghala hilo unavyoendelea.

 

Dk. Mollel ametumia fursa ya ziara hiyo, kuwapongeza watumishi wa MSD Mtwara kwa juhudi na kujituma kwao katika kuwahudumia wananchi licha ya changamoto ya udogo wa ghala uliopo.

 

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jingu, amewataka watumishi hao kutobweteka na kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwani serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto zinazowakabili, ikiwemo tatizo la ufinyu wa ghala hali inayosababisha ujenzi wa ghala jipya na la kisasa.

 

Ameongeza kuwa ziara yao katika Kanda hiyo, ni kudhihirisha kwamba wanatambua changamoto iliyopo, hivyo kwa kushirikiana na viongozi wengine wanaendelea kufanyia kazi changamoto hiyo, ili kupata tatuzi.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amesema taasisi hiyo kupitia mpango mkakati wake, iko katika mchakato wa maboresho ya huduma na utendaji kazi, ikiwa ni pamoja na ujezi wa maghala kwenye kanda tofauti nchini.

 

Amesema hatua hiyo itapanua  wigo na uwezo wa MSD katika kuwahudumia wateja wake kikamilifu, kwani itaongeza uwezo wa MSD kuhifadhi bidhaa za kutosha kwaajili ya wateja na kupunguza gharama kubwa za uendeshaji.

 

Mavere amezitaja Kanda hizo zitakazofikiwa na maboresho ya maghala kuwa ni pamoja na Mtwara, Mwanza, Kagera na Dodoma kwa kuanzia na baadaye kuangalia kanda nyingine zenye uhitaji.

Kamati ya Bunge ya Afya na UKIMWI Yataka Madeni ya MSD Yalipwe Haraka

WhatsApp_Image_2023-09-13_at_4.35.04_PM.jpeg

Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam Akifafanua Jambo kwa Waandishi wa Habari Baada ya Kumalizika

kwa Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge

 

Dar es Salaam.

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI imezitaka taasisi zinazodaiwa na Bohari ya Dawa(MSD) kulipa madeni hayo ambayo kwa ujumla yanafikia zaidi ya Sh.bilioni 20 na miongoni wanaodaiwa fedha ni Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI.

Ushauri huo umetolewa leo Septemba 13, 2023 jijini Dar es Salaam na Kamati hiyo baada ya kufanya ziara ya kutembelea maghala ya MSD Mabibo na Keko ambapo pia wameelezwa kufurahishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na bohari hiyo kuhudumia wananchi katika kununua, kuhifadhi na kusambaza dawa na vifaa tiba kwa wastani wa zaidi ya asilimia 90.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Stanslaus Nyongo wakati akitoa majumuisho ya ziara hiyo ya Wabunge wa Kamati ya Bunge ya Afya na Ukimwi amesema wamefurahishwa na mikakati ya bohari hiyo lakini ni vema wanaodaiwa wakalipa madeni ili MSD iendelee kutoa huduma zake.

"Tumepata taarifa mbalimbali za MSD namna ambavyo wamejipanga kutoa huduma zao kwa wananchi lakini kunachangamoto ya madeni ambayo wanadai kwa wateja wao, hivyo tunashauri madeni hayo yalipwe...

" Hata hivyo katika kujadili madeni ambayo MSD wanadai kwa wateja wao tumeelezwa yanachelewa kwasababu nao wanasubiria kulipwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya( NHIF).

"Katika ziara yetu tunatarajia kwenda Bima ya Afya hivyo tutazungumza nao ili waweze kulipa fedha ambazo wanadaiwa.Kwa hiyo hili ni jambo ambalo tutalizungumza na kupata muafaka " amesema Nyongo.

Kuhusu maombi ya MSD kuomba mtaji kwa Serikali, Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema serikali ipo katika hatua ya mwisho ya kuipatia mtaji MSD na Bunge litaendelea kupigania uwezeshaji huo ufikiwe kwa haraka lengo likiwa ni kuijengea uwezo taasisi hiyo kwa maslahi ya taifa.

Amefafanua hali hiyo ndio msingi wa matokeo ya maborehso ya huduma bora za afya hatua ambayo pia itakayochea bohari kujenga maghala yake na kupunguza mzigo wa gharama ya kukosi, kuagiza, kusambaza na kuzalisha dawa na vifaa tiba ipasavyo.

"Kamati imejiridhisha namna MSD ilivyojipanga kimkakati katika uzalishaji wa dawa na kuweza kukua kwa taasisi hiyo kulingana na mahitaji yaliyopo.Hivyo wakati hayo yakiendelea ni vema wanaodaiwa na Bohari hiyo kanda ya Mashariki wakalipa madeni."

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dk.Godwin Mollel ameelezea hatua kwa hatua juhudi zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuiwezesha bohari hiyo na sekta ya afya kwa ujumla na kuhusu deni ambalo MSD wanadai kwa Hospitali ya Muhimbili na MOI.

Akielezea madeni hayo amesema tayari maelekezo yalishatolewa kuwa ndani ya siku 60 tangu huduma kufanyika deni lilipwe, hivyo hayo ni maagizo huku akifafanua watazungumza na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili nao walipe fedha wanazodaiwa na hospitali hizo.

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai, ameeleza kwamba kwa sasa bohari imefurika shehena za dawa na vifaa tiba ambavyo vinaendelea kupakuliwa ukiwa ni mzigo ulioagizwa hivi karibuni.

“Kamati imekuja wakati mzuri tumetoka katika uagizaji tupo katika kupokea mzigo mkubwa wa vifaa vya afya, sasa miradi yote iliyokuwa na changamoto hususani ya vifa tiba kuna shehena ya kutosha kontena zinaendelea kushusha mizigo na tumewaeleza tulipotoka tulipo na tunapokwenda.

“Hatuongelei mikakati tena tupo katika utekelezaji tumeboresha mikataba ya uagizaji bidhaa, upatikanaji na uhusiano wetu na washitiri kwa kugatua MSD, kuboresha uwajibikaji na miundombinu kwa kujenga maghala mapya ambapo Dar es Salaam tunalipa bilioni 2 kwa mwezi kukodi ghala moja hivyo ni lazima tujenge ya kwetu,”amesema

Aidha amesema kutokana na kupungua kwa mtaji wa bohari hiyo Serikali inaendelea na hatua za utekelezaji za kuipatia fedha ambapo Wizara ya Fedha ipo katika mchakato wa mwisho na matumaini yaliyopo ni makubwa lengo ni kuhakikisha huduma za afya nchini zinakidhi mahitaji yaliyopo.

Mavere amesema katika kuhakikisha bohari hiyo haiwi mzigo kwa serikali wanaendelea na mchakato wa kushirikisha sekta binafsi katika uzalishaji.

Awali Meneja wa MSD Kanda ya Mashariki Betia Kaema alisema kanda hiyo inayohudumia Mikoa ya Pwani na Zanzibar ina changamoto kubwa ya kukosa eneo la ghala linalokidhi viwango na madeni wanayowadai wateja wao.

“Kamati imetushauri kufuatilia kwa kina madeni yaliyopo kwa kuwa yanakua kwa kasi, hadi sasa kanda inadai zaidi ya sh. bilioni 20 na sisi ili tupate dawa na huduma ziendelee ni lazima tulipe supply...

"Tumepokea maelekezo na tutaendelea kuzungumza na tunaowadai waweze kutulipa na sisi tuweze kujiendesha,”ameseema Kaema na kusisitiza kwa sasa usambazaji dawa na vifaa tiba umeimarika na hivyo kupunguza malalamiko kama ilivyo huko nyuma.

Maboresho ya Mnyororo wa Usambazaji Bidhaa za Afya Nchini

IMG-20230720-WA0360.jpg

Magari ya Usambazaji ya MSD Yakiwaa Kwenye Majukumu Yake ya Usambazaji wa

Bidhaa za Afya Nchini.

Dodoma.

Ongezeko la usambazaji wa bidhaa za afya unaofanywa na Bohari ya Dawa (MSD) tangu Mwaka wa Fedha 2022/23 baada ya mapitio ya mnyororo wa ugavi na mapendekezo ya maboresho ya usambazaji bidhaa za afya, umepelekea kuimarika kwa upatikanaji wa bidhaa hizo nchini.

Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa MSD, Hassan Ally Ibrahim ameyasema hayo leo katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO uliopo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maboresho ya mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya ikiwa ni mwendelezo wa taasisi kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Ibrahim amesema kuwa, hadi kufikia mwezi Juni 2023, MSD ilikuwa na mikataba ya muda mrefu 238 yenye jumla ya bidhaa za afya 2,004 ukiwa ni mkakati maalumu wa kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya ambapo katika kuendana na kasi ya ongezeko la vituo vya afya inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, MSD imekuwa ikifanya mawasiliano na balozi za Tanzania zilizopo China, Algeria, Korea ya Kusini, Urusi na maeneo mengine duniani ili kuweza kufanya utambuzi wa wazalishaji, wawekezaji na kuwezesha ununuzi wa bidhaa za afya kwa uhakika, ubora na gharama nafuu.

 “Serikali kupitia MSD ilianza rasmi kutekeleza jukumu la usambazaji wa bidhaa za afya mara sita badala ya mara nne kwa mwaka kwa vituo vyote vya umma vya kutolea huduma za afya kwa mwaka wa fedha 2022/23. Usambazaji huu unaondoa tatizo la upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuhakikisha kwamba vituo vyote vinapelekewa bidhaa za afya hadi mlangoni mwa vituo vya kutolea huduma za afya kila baada ya miezi miwili,” amesema Meneja Ibrahim.

Katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali kupitia Bohari ya Dawa ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 157.56 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya za vituo vya kutolea huduma za afya ambapo kiasi hicho cha shilingi bilioni 157.56 ni kiasi cha juu kuwahi kutolewa na Serikali kupitia Bohari ya Dawa tokea kuanzishwa kwake miaka 30 iliyopita. Kiasi hicho ni sehemu tu ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ununuzi wa bidhaa za afya.

MSD Yabainisha Mikakati Yake kwa Mwaka 2023/2024

IMG-20230807-WA1947.jpg

Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa MSD, Hassan Ally Ibrahim, Akiongea na Vyombo vya Habari Juu ya Maboresho ya MSD na Mipango Mikakati ya MSD Kwa Mwaka wa Fedha, 2023/2024, Katika Ukumbi wa Habari Maelezo Jijini Dodoma.

Dodoma.

Bohari ya Dawa (MSD) imebainisha kwamba katika Mwaka wa Fedha 2023/24, inatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya zikiwemo dawa, vifaa tiba na vitendanishi, kupitia mikakati maalumu iliyowekwa na Bohari hiyo.

Mikakati hiyo imeelezwa leo na Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa MSD, Hassan Ally Ibrahim katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO uliopo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maboresho ya mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya ikiwa ni mwendelezo wa Taasisi kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24.

“Katika kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya, kitakachofanyika cha kwanza ni kuhimiza matumizi ya takwimu ili kufahamu mahitaji, wakati na maeneo ambayo bidhaa za afya zinahitajika, maeneo mengine ya msingi ambayo kwa sasa MSD inayafanyia kazi ni kuimarisha mfumo mzima wa ununuzi kwa kuangalia vizuri mikataba ili bidhaa za afya zisikosekane”.

“Vilevle, tutahimiza ushirikiano na wazalishaji wa ndani ambapo tutatoa fursa kwa kuzingatia misingi ya kisheria na kununua bidhaa kutoka kwao,” amesema Meneja Ibrahim.

Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na miundombinu ya utunzaji wake kupitia fedha zitakazotolewa na Serikali, kuanza uzalishaji wa mipira ya mikono kwa kiwanda kilichopo katika Kijiji cha Idofi, mkoani Njombe ambacho kipo mbioni kukamilika, kuanza kutekeleza miradi ya uanzishaji wa viwanda vya bidhaa za afya eneo la Zegereni, mkoani Pwani na uanzishaji wa viwanda vya Pamba tiba.

Mikakati mingine ni pamoja na  maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa pamoja na bidhaa za pamba tiba na kuanza ujenzi wa maghala ya kisasa katika mikoa ya Dodoma, Mtwara na Kagera kwa lengo la kuongeza nafasi za kuhifadhi bidhaa na kuimarisha ubora wa bidhaa za afya, ambapo ujenzi wa maghala hayo unatarajiwa kuanza mwezi Agosti 2023.

Utekelezaji wa majukumu hayo ya MSD unaenda sambamba na utekelezaji wa maelekezo ya maboresho ya utendaji yaliyotolewa na Rais, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, wakati alipoteua uongozi mpya wa Bohari hiyo.

Ameongeza kuwa MSD inapitia mifumo yote ya uendeshaji ikiwemo mnyororo wa ugavi, usimamizi na TEHAMA ili kuendana na kasi ya ongezeko la ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya, vinavyojengwa na Serikali na kuhakikisha malengo ya Serikali katika upatikanaji wa bidhaa za afya yanafikiwa.

MSD Yasambaza Vifaa Tiba vya Kisasa Wilayani Mafia

WhatsApp_Image_2023-08-15_at_13.30.35.jpeg

Afisa Huduma kwa Wateja wa Kanda ya Dar es Salaam Bi. Diana Kimario Akiwa Kwenye Picha ya Pamoja na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mafia (kushoto) na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mafia(kulia), Alipotembelea Wilayani Mafia kwa ajili ya Makabidhiano ya Vifaa Tiba

 

 

Kagera.

BOHARI ya Dawa (MSD) imesema usambazaji wa dawa na vifaa vya kisasa Kisiwani Mafia mkoani Pwani umefanikiwa kupunguza rufaa za wagonjwa kutoka kisiwani humo kwenda kutibiwa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana kisiwani Mafia Afisa Huduma kwa Wataeja wa MSD wa kanda hiyo Diana Kimario, alisema Bohari hiyo imefanikiwa kupunguza rufaa za wagonjwa kutoka kisiwani Mafia kwenda jijini Dar es Salaam kwa kufunga vifaa tiba vya kisasa hususani vya maabara na upasuaji.

“Wilaya hii ina vituo vya afya 25 ambapo vituo 21 vipo Mafia na vituo vine vipo katika visiswa vidogo, ambapo vifaa vilivyosambazwa na MSD vitafanikisha kupunguza changamoto ya rufaa kwa wagonjwa waliokuwa wakisafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya huduma,” alisema.

Alisisitiza kuwa wamefanikiwa kusambaza Xray mashine, vitandaa vya kuchangia damu, mashine za kusaidia upumuaji, jenereta kubwa na ndogo na vifaa vingine vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 450,” alisema.

Diana alisema hatua hiyo imefikiwa kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Rais Dk.Samia kwa hospitali hiyo kuwa na majengo ya kisasa yanayokidhi vifaa vilivyofungwa hususani jengo la dharula na wagonjwa mahututi (ICU).

Alisema, pamoja na mafanikio hayo wamekuwa wakikutana na changamoto ya usafirishaji wa dawa na vifaa tiba kutokana na tozo wanazokutana nazo bandarini hivyo wanaiomba serikali kuona namna ya taasisi husika ikiwemo wilaya, MSD na bandari kukaa pamoja na kutoa msamaha kwa bidhaa za afya.

“Kuleta gari ya dawa na vifaa tiba Mafia ni gharama unalipia kivuko na kodi kwa bandari na Nyamisati na Mafia na iwapo tutashindwa kulipia inatulazimu kushusha mzigo na kupakia katika meli na wanapofika Mafia, gari ndogo za serikali hutafutwa au za kukodi ili kusambaza ambapo usambazaji unachukua muda mwingi.

“Kutokana na hali hiyo MSD Kanda ya Dar es Salaam tumeomba kukutana na wenzetu uongozi wa wilaya, Mbunge, uongozi wa kivuko na bandari waone namna ya kusamehe kodi katika bidhaa za afya,” alisema

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Maulid Majala alisema hospitali hiyo imepokea zaidi ya sh.milioni 550 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya mawili na sh.bilioni 1.39 kwa ajili ya vifaa tiba hivyo anatoa wito kwa watumishi kuhakikisha uwekezaji huo unaendana na thamani ya huduma zinazotolewa.

Alisema ujenzi wa majengo hayo na vifaa vya kisasa ni muhimu, kwa kuwa awali walikuwa wakikutana na wagonjwa wa dharula hususani wa ajali inawaladhimu kuwapa rufaa kutokana na hospitali hiyo kukosa vitendea kazi.

Dkt.Majala alieleza ujio wa bidhaa hizo za afya na upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 60 hadi 90 umeboresha utoaji wa huduma kisiwani Mafia.

Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Mafia ambaye ni daktari bingwa wa wanawake Dk.Said Maya, alisema kutokana na mazingira ya kisiwa hicho wanaishukuru MSD kwa kazi kubwa inayoifanya kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinafika hadi vituoni bila kujali changamoto za mazingira yaliyopo.

Lock full review www.8betting.co.uk 888 Bookmaker