Aller au contenu principal
new

YALIYOJIRI LEO AGOSTI 15, 2025 KATIKA MKUTANO WA KATIBU MKUU WA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO NA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI BW. GERSON MSIGWA NA WAANDISHI WA HABARI JIJINI DODOMA.

Bohari ya Dawa (MSD) ni ni taasisi inayomilikiwa na Serikali iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Sheria ya Bohari ya Dawa Na.13 ikiwa na majukumu manne (4); Uzalishaji, Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na vile vya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya. Katika kipindi cha awamu ya sita ya uongozi, vituo vya kutolea huduma za afya vinavyohudumiwa na MSD vimeongezeka na kufikia vituo 8,776 mwaka 2024/2025 kutoka vituo 7,095 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la vituo 1,681 ambapo ni ongezeko la asilimia 24. 

Bohari ya Dawa imeendelea kuhudumia vituo hivi kupitia Kanda zake 10 zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya na Iringa. 

2.0     Mafanikio ya Bohari ya Dawa

Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2025, Bohari ya Dawa imepata mafanikio mengi katika kutekeleza majukumu yake. Baadhi ya mafanikio yamepatikana katika maeneo yafuatayo: -

2.1     Mwenendo wa Fedha zinazotengwa na serikali kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya

Chanzo kikuu cha fedha za ununuzi wa bidhaa za afya kwa vituo vya kutolea huduma za afya ni fedha inayotengwa na Serikali Kuu. Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali imeweza kutoa kiasi cha shilingi bilioni 196.3 kati ya bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 200 sawa na asilimia 98 ya fedha yote ya vituo kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya. Hii ni fedha nyingi kutolewa katika kipindi chochote tokea kuanzishwa kwa Bohari ya Dawa. 

Kwa kipindi cha miaka minne, Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitenga bajeti ya ununuzi wa bidhaa za afya za vituo vya kutolea huduma za afya kupitia Bohari ya Dawa ya kiasi cha shilingi bilioni 805. Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2025, MSD imepokea jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 642.1 sawa na asilimia 80 ya fedha za ununuzi wa bidhaa za afya kwenye vituo vya kutolea Huduma za Afya kwa kipindi cha miaka 4.

Grafu Na. 1: Mwenendo wa fedha zilizotengwa na zile zilizopokelewa

 

2.2     Makusanyo Ya Fedha Taslimu (Cash Collection)

Pamoja na fedha za ununuzi wa bidhaa za afya zinazotengwa kwenye Bajeti Kuu ya Serikali kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya, MSD hukusanya fedha (Cash collection) kutoka vituoni ambazo zinatoka kwenye vyanzo vingine vya vituo husika. 

Kwa mwaka wa fedha 2024/25, makusanyo ya MSD yalikuwa ni makubwa kuliko kipindi chochote ambapo kiasi cha shilingi bilioni 184.2 sawa na asilimia 70 ya lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 264.5 zilikusanywa. Kati ya kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi kufikia tarehe 30 Juni 2025, MSD imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 397.6 ikilinganishwa na lengo la kiasi cha shilingi bilioni 795.0. Kiwango cha ukusanyaji wa fedha hizi kimeendelea kukua mwaka hadi mwaka. Mchanganuo wa ukusanyaji kwa kila mwaka ni kama inavyooneshwa katika Grafu hapa chini;

Chart

Grafu Na. 2: Mwenendo wa Makusanyo taslimu

 

Ongezeko la makusanyo ya fedha limetokana na maboresho yanayoendelea yaliyowezesha kupatikana kwa bidhaa za afya kwa uwingi katika maghala ya MSD zinazoendana na mahitaji ya vituo, kuongezeka kwa uwezo wa wateja kulipia bidhaa kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali na kuimarika kwa mahusiano kati ya MSD na wateja.

2.3     Kuongezeka kwa Mapato ya MSD

Sheria ya Bohari ya Dawa inaeleza kwamba MSD itakuwa inajiendesha kwa mfumo wa uzungushaji wa fedha (revolving fund) ambapo utaratibu huu unazingatia gharama ya uendeshaji, ununuzi wa bidhaa za afya na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya na uendeshaji wa Taasisi unakuwa endelevu. Kupitia mfumo huu,Serikali imeweka msingi wa kuhakikisha MSD haipokei fedha yoyote ya ruzuku kutoka Serikalini ikiwemo mishahara ya watumishi.

Kutokana na maboresho yanayoendelea na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika vituo vya kutolea huduma za afya, mapato ya Bohari ya Dawa yameendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 315.1 kwa mwaka wa fedha 2021/22, hadi kufikia shilingi bilioni 640 kwa mwaka wa fedha 2024/25 ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 325 ambayo ni sawa na asilimia 103.1 kama inavyoonekana hapa chini; 

Grafu Na. 3: Mwenendo wa Mapato

 

Chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa mapato haya ni kuongezeka kwa mapato yanayotokana na mauzo ya bidhaa za kawaida ambapo bidhaa zilizosambazwa zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 315.8 mwaka 2023/24 hadi kufikia shilingi bilioni 429.1 mwaka 2024/25 ikiwa ni ongezeko la asilimia 35.8. Hii maana yake ni kuwa taasisi imeongeza uwezo wa kuzalisha mapato yake kutokana na shughuli za msingi (core functions) kulinganisha na yale yanayotokana na miradi ya wahisani. Ukuaji huu unaifanya taasisi kuwa stahimilivu na kuendelea kuhakikisha kuwa bidhaa za afya zinawafikia Watanzania wote.

Kwa upande wa matumizi ya ununuzi wa bidhaa za afya nayo yameongezeka kutoka kiasi cha shilingi bilioni 285.4 mwaka 2021/22 hadi kufikia kiasi cha shilingi bilioni 567.9 mwaka 2024/25. Matumizi haya yameongezeka kutokana na ongezeko la fedha zinazoelekezwa kwenye ununuzi wa bidhaa za kawaida ambapo zilipanda kutoka shilingi bilioni 229.3 mwaka 2021/22 hadi kufikia shilingi bilioni 468.5 mwaka 2024/25.

 

2.4     Utimizaji wa Mahitaji ya Bidhaa za Afya

Hali ya utimizaji wa mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya umeendelea kuimarika ambapo hadi kufikia mwezi Juni 2025, hali ya utimizaji wa mahitaji ilikuwa ni  asilimia 79 ikilinganishwa na asilimia 39 iliyorekodiwa mwaka wa fedha 2021/22. Ongezeko hili linatokana na maboresho maalum ya kiutendaji yanayoendelea kutekelezwa ndani ya taasisi kufuatia maelekezo ya Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa mwezi Machi 2022 ikiwemo uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi na mabadiliko ya Mkurugenzi Mkuu, Serikali kuendelea kuhakikisha kunakuwepo na fedha ya kutosha ya vituo kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya na vituo kuendelea kuwezeshwa kufanya ununuzi wa bidhaa za afya. 

Grafu Na. 4: Utimizaji wa mahitaji

 

2.5     Ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani

Serikali inatambua umuhimu wa kusimamia na kukuza uzalishaji wa bidhaa za afya kutoka viwanda vilivyopo nchini. Baadhi ya faida zinazopatikana kwa kufanikisha uzalishaji kutoka kwa viwanda nchini ni pamoja na kuhakikisha usalama wa masuala ya kiafya pale inapotokea dharura za magonjwa au majanga mbalimbali, kutengeneza ajira, na kulinda akiba ya fedha za kigeni. Katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2021/22 mpaka mwaka 2024/25, Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeendelea kuongeza thamani ya bidhaa za afya zinazonunuliwa kutoka kwa wazalishaji nchini. Kwa Mwaka wa Fedha 2021/22, bidhaa za afya za thamani ya shilingi billioni 15.9 zilinunuliwa kutoka kwa wazalishaji wa ndani. Thamani hii imeendelea kuongezeka na kufikia shilingi billioni 98.72 kwa mwaka wa fedha 2024/25 kama inavyoonekana kwenye grafu hapa chini.

Grafu Na. 5: Thamani ya bidhaa zilizonunuliwa

 

2.6     Ununuzi na Usambazaji wa Vifaa Tiba

Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye kuongeza miundombinu ikiwemo ujenzi wa vituo vipya, kuboresha vituo vilivyokuwepo na kuongeza aina za huduma za afya kwenye vituo mbalimbali nchini. Kwa kipindi cha miaka minne, MSD imefanya ununuzi na usambazaji wa vifaa na vifaa tiba vinavyohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi vituo vinavyotoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini. Vifaa vingi katika hivi hutumika kufanya uchunguzi na kuwezesha vituo vya kutolea za afya kutimiza majukumu yao ipasavyo. Baadhi ya vifaa vilivyosambazwa ni pamoja na mashine za usingizi, CT- Scan, MRI 3T, Ultrasound mashine, na digital X-Ray vyenye jumla ya shilingi bilioni 429.2. Kwa mwaka wa fedha 2021/22, Bohari ya Dawa ilikuwa ikisambaza vifaa tiba vya thamani ya shilingi bilioni 18.1 pekee. Hadi kufikia mwaka wa fedha 2023/24, MSD iliweza kusambaza vifaa tiba vya thamani ya shilingi bilioni 193.1 kwa mchanganuo unaoneshwa hapa chini: -

 

Grafu Na. 6: Thamani ya vifaa vilivyonunuliwa

 

Grafu hapo juu inaonesha uwekezaji mkubwa ambao Serikali inafanya mwaka hadi mwaka ili kuhakikisha huduma za afya zinakuwa za uhakika na zinapatikana karibu na wananchi.

2.7     Usambazaji wa Bidhaa za Mradi Msonge.

Upatikanaji wa bidhaa za Mradi Msonge zinazohusu magonjwa maalum ya UKIMWI, Malaria, Kifua Kikuu na Ukoma zimeendelea kutolewa bure. Bohari ya Dawa imeendelea kutekeleza jukumu hili kwa kuhakikisha bidhaa hizi zinafika kwa walengwa. Katika kuimarisha utekelezaji endelevu wa Mradi Msonge, Bohari ya Dawa iliongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huu kutoka asilimia 18 mwaka 2022 na kufikia asilimia 97 mwezi Desemba mwaka 2024 ambayo ilikuwa ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Global Fund mzunguko wa sita (GC6). 

Aidha, katika kuhakikisha hakuna athari yoyote inayotokea kutokana na mabadiliko ya sera za nchi za nje za wadau wa maendeleo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili bidhaa zote zinazohusu magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria ziweze kuendelea kupatikana nchini. Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeelekeza fedha zote zinazohitajika jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 142 kufanikisha ununuzi huo hivyo na kuondoka kabisa uwezekano wa changamoto ya ukosefu wa bidhaa hizo. Hatua hii inalenga kuendelea kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hizi kwa uhakika na wakati wote.

3.0     Utekelezaji wa Miradi Maalum ya Vipaumbele

3.1     Mpango wa Usambazaji wa Mashine za Uchujaji damu “Dialysis”

Serikali kupitia Bohari ya Dawa inatekeleza mpango maalumu wa kuongeza upatikanaji wa huduma za uchujaji wa damu ikiwa ni sehemu ya matibabu ya figo, hivyo kupunguza gharama za huduma hiyo. Kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya awamu ya sita, hadi kufikia mwezi Agosti 2025, idadi ya mashine imeongezeka na kufikia mashine 137 kutoka mashine 60 na hivyo kuongeza idadi ya hospitali zilizopokea mashine kutoka Bohari ya Dawa kutoka hospitali 6 zilizokuwepo mwaka wa fedha 2021/22 na kufikia hospitali 15 mwaka 2024/25. Uwekezaji huu uliofanyika umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 7.7.

Katika hospitali hizi, hospitali 11 zimeanza kutoa huduma na hospitali 4 zipo katika hatua ya matengenezo. Baadhi ya hospitali zinazotoa huduma ni pamoja na Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Amana, Mwananyamala, Temeke, Morogoro, Katavi, Tumbi, Chato, Sekoe Toure na UDOM Hospitali.

Mkakati huu wa usambazaji wa mashine za dialysis unalenga kupunguza gharama ambapo kwa sasa gharama zinazotozwa ni kati ya shilingi 200,000 na shilingi 230,000 na matarajio ni kuweza kupunguza na kuwa chini ya shilingi 100,000 kwa ‘session’ moja. Mkakati huu unatekelezwa chini ya uratibu imara wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na hospitali zinazotoa huduma za hemodialysis ambapo kifurushi cha msingi cha vifaa vinavyotumika katika hemodialysis kwa ajili ya vipindi 100 (hemodialysis consumables basic kit content for 100 sessions) kimeanzishwa. Kifurushi hiki kina jumla ya bidhaa muhimu 15 kwa kila kipindi kimoja cha dialysis.

Picha 1: Baadhi ya mashine za kusafisha damu (Dialysis)

3.2     Usambazaji wa Bidhaa za Afya za Kinywa

Usambazaji wa bidhaa za afya ya kinywa na meno umeendelea kuimarika katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita ambapo Bohari ya Dawa imeendelea kuhakikisha bidhaa za afya ya kinywa na meno zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia Bohari ya dawa imesambaza bidhaa za afya za kinywa na meno zenye thamani ya shilingi bilioni 9.98 kutoka kusambaza bidhaa za afya za kinywa na meno zenye thamani ya shilingi milioni 254.7 kwa mwaka 2021/2022.  Katika kipindi cha miaka minne mfululizo bidhaa za afya za kinywa na meno zenye thamani ya shilingi bilioni 21.5 zimesambazwa, ambapo shilingi bilioni 17.87 ni thamani ya viti vya kutolea huduma za kinywa na meno na pamoja na mashine za mionzi ya kinywa na meno ambayo ni sawa na asilimia 83. Katika gharama hii, viti vya huduma za kinywa na meno vimegharimu shiling bilioni 13.8 na kuwezesha kusambazwa kwa viti 647 na mashine za kisasa za mionzi za kinywa na meno zikiwa ni 331 zenye thamani ya shilingi bilioni 4.07. Bidhaa hizi zimesambazwa katika hospitali za ngazi ya Mkoa na Wilaya. Mwenendo wa thamani ya bidhaa za kinywa na meno zilizosambazwa kwa mwaka ni kama inavyoonekana katika grafu ifuatayo;

Grafu Na. 7: Thamani ya bidhaa za kinywa na meno zilizosambazwa

 

Grafu hii imeonesha ongezeko la bidhaa za meno na kinywa kwa kila mwaka hivyo kuonesha uwekezaji mtambuko unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika maeneo mbalimbali ya huduma ambapo hapo awali huduma za aina hii zilikuwa adimu maeneo mengi nchini.

3.3     Usambazaji wa Bidhaa za Mama na Mtoto (CEMONC)

Katika kuboresha afya ya mama na mtoto kwa kutoa huduma za dharura za uzazi pingamizi na huduma za awali kwa watoto wachanga, Serikali kupitia Bohari ya Dawa katika kipindi cha miaka minne imenunua na kusambaza bidhaa za afya, kwa ajili ya kuboresha vituo vya afya 316 na kuhakikisha vinatoa huduma ya dharura ya uzazi na mtoto - Comprehensive Emergency Obstetric and New-born Care - CEmONC. Bidhaa zote za afya 414 zenye thamani ya shilingi 100,182,390,897.40 zimekwisha sambazwa na kusimikwa kwenye vituo hivyo vya kutolea huduma za afya nchini. 

3.4     Ufanisi wa Usambazaji kwa Kuzingatia Muda Uliowekwa.

Katika kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana wakati wote kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeendelea kufanikisha usambazaji wa bidhaa za afya nchi nzima kwa mizunguko sita (vituo kupelekewa bidhaa kila baada ya miezi miwili) kutoka mizunguko minne (vituo kupelekewa bidhaa kila baada ya miezi mitatu) na hivyo kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya zinakuwa na dawa toshelevu muda wote.

Aidha, Bohari ya Dawa imeendelea kuboresha usambazaji wa bidhaa za afya kwa wakati kwa asilimia 98 kutoka katika maghala yake hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya. Asilimia hii imeongezeka kutoka asilimia 23 iliyoripotiwa mwaka 2021/2022.

4.0     Usimamizi wa Sheria, Kanuni na Taratibu, na Miongozo Mbalimbali

Bohari ya Dawa imeendelea kufanya maboresho kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni, ikiwemo miongozo mbalimbali hivyo kuwezesha kupungua kwa hoja za kikaguzi kutoka hoja 130 mwaka 2020/21 na kufikia hoja 44 mwaka wa fedha 2023/24. Ili kuondokana na hoja hizi, hatua mbalimbali zinachukuliwa ikiwemo usimikaji wa mifumo ya TEHAMA, ujenzi wa maghala, maboresho na uimarishaji wa usimamizi wa kiutendaji.

5.0     Maboresho ya Utendaji

Mwaka 2021/22, utendaji wa Bohari ya Dawa ulikuwa ukilalamikiwa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya vikiwemo vituo vya kutolea huduma za afya kutokana na mapungufu yaliyokuwepo. Malalamiko yalihusu kutopatikana kwa bidhaa za afya ashiria toshelevu na nyinginezo, uchelewaji wa kuhudumia mahitaji ya wateja ikiwemo usambazaji wa bidhaa husika, mapungufu ya mfumo wa utawala bora na usimamizi wa utendaji. Hivyo, utendaji wa MSD kwa wakati huo haukuweza kuakisi matarajio ya wadau na ukuaji wa sekta ya afya pamoja na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia yanayohusu bidhaa za afya

Hivyo, mnamo mwezi Machi 2022, Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa maelekezo ya mfumo na utendaji wa Bohari ya Dawa ufanyiwe mapitio na ufumuliwe wote ili kuendana na mahitaji ya sasa ya vituo vya kutolea huduma za afya na kujiendesha kwa ufanisi. Kutokana na maelekezo hayo, Bohari ya Dawa ilitafuta Mshauri Elekezi anayejitegemea “Deloite Consulting Limited ili aweze kufanya mapitio na kushauri namna bora ya uendeshaji wa Taasisi. Kutokana na changamoto zilikuwepo, baadhi ya maeneo yalifanyiwa mapitio ni kama yalivyoainishwa hapa chini:

5.1     Mapitio ya Muundo wa Taasisi

Maboresho ya Muundo wa Bohari ya Dawa yalilenga kuboresha utendaji ndani ya Taasisi ili kuwa na Muundo unaendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya afya kwa lengo la kuboresha utendaji ndani ya MSD. Hivyo, uongozi wa Bohari ya Dawa kupitia Mshauri Elekezi ulifanya tathmini ya maeneo mbalimbali ikiwemo uwezo wa Muundo wa Taasisi (Organization Structure) uliokuwepo kuwezesha Taasisi kutekeleza Majukumu ya Msingi (Core Functions) kwa ufanisi. Baada ya kupitia, kuchakata na kutathmini mapendekezo ya Mshauri Elekezi, Bohari ya Dawa ilianza hatua za maboresho ya Muundo wa Taasisi na Kazi za Kurugenzi, Vitengo na Sehemu. Baada ya mapitio hayo, mnamo mwezi Februari 2025, Msajili wa Hazina aliridhia Muundo Mpya wa Bohari ya Dawa.

Muundo huu mpya wa taasisi umefanya mabadiliko katika maeneo yafuatayo; Kuanzisha Kurugenzi mahsusi kwa ajili ya Huduma kwa Wateja na kuweza kuwa na sehemu maalum ya wateja wakubwa, Kuanzisha Kurugenzi ya Usambazaji ambapo Kurugenzi hii  itakuwa inatekeleza jukumu la Ugomboaji na Usafirishaji, Kupanga idara ya Ununuzi ambao kwa sasa itazingatia hatua za ununuzi badala ya bidhaa itakayokuwa inanunuliwa. Maboresho haya, yanatarajiwa kuongeza ufanisi na kutoa kutoa fursa kwa taasisi kuimarisha matumizi ya rasilimali mbalimbali za taasisi na kuongeza tija. 

Pamoja na maboresho hayo, taasisi imetambua umuhimu wa taasisi kujiendesha kibiashara kwa kuanzisha Kurugenzi ya Mipango na Uwekezaji ili kuweza kutambua fursa za uwekezaji na kuwezesha taasisi kushiriki katika fursa mbalimbali hasa kwenye maeneo ya viwanda na usambazaji wa bidhaa za afya. 

5.2     Mabadiliko ya Watumishi

Katika hatua za kuboresha utendaji kazi, Bohari ya Dawa ilifanya mabadiliko ya muundo wa utumishi (scheme of service) na kuongeza kada muhimu, kama Wataalamu wa tiba ya miyonzi, Wahandisi wa Vifaa Tiba (Biomedical Engineers), Kinywa na Meno, na Maabara (Laboratory Scienticists). Ongezeko la kada hizi linalenga kuhakikisha kuna uelewa wa mawasiliano kati ya vituo vya kutolea huduma za afya na watumishi waliopo Bohari ya Dawa.Katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2021 hadi Juni 2025, jumla ya watumishi 113 walihamishiwa Taasisi nyingine za umma, na watumishi 100 walihamia bohari ya dawa kwa lengo la kuwezesha taasisi kufikia malengo yake.

5.3     Mapitio ya Mfumo wa Tehama

Bohari ya Dawa imefanya mageuzi makubwa katika mifumo ya TEHAMA kupitia mradi wa kimkakati wa mageuzi ya kidijitali (i.e. MSD Digital Transformation). Bohari imedhamiria kuifanya TEHAMA moja ya nguzo kuu ya usimamizi wa Taasisi na myororo wa ugavi wa dawa. Kupitia mradi huu Bohari imefanya mapitio makubwa ya mifumo yake yote na kusasisha mifumo iliyopitwa na wakati na kujenga mifumo ya TEHAMA ya kisasa (ikiwemo fursa ya kutumia  akili mnemba). Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kwenye TEHAMA ni kama yafuatayo;

  1. Kuongeza matumizi ya mifumo kutoka 62.5% mwaka 2021 hadi kufikia 98.5% mwezi Juni 2025 kwa michakato yote ya msingi ya kiutawala inayowezesha manunuzi, uhifadhi, na usambazaji wa bidhaa za afya. Aidha, ukijumuisha mifumo ya kutuma ankara kwa vituo vya kutolea huduma za afya, kiwango cha jumla cha matumizi ya TEHAMA katika mnyororo mzima wa ugavi kimefikia asilimia 74. Hii inaonesha hatua kubwa iliyopigwa kuelekea mnyororo wa ugavi wa kidijitali. Bohari ya dawa imedhamiria na inaendelea na juhudi za kufikia matumizi ya karatasi 0% (Paperless Office) hadi ifikapo Oktoba 2026. Bohari ya Dawa imehakakisha michakato yake yote ya ndani, hasa ile ya ununuzi, inafanyika bila makaratasi kupitia dirisha la MSD Connect. MSD pia ni mdau mkubwa wa mfumo wa kitaifa wa manunuzi wa NeST na katika kipindi cha 2021-2025.
  2. Kuweza kubadlishana taarifa na jumla ya mifumo saba (7) ya kisekta, fedha na wadau wa maendeleo ambapo imeongeza ubora wa taarifa, ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
  3. Kuongeza uwazi na ufanisi wa huduma zake kwa wateja kupitia mfumo wa wazi wa wateja kujihudumia (Client Self Service Portal) na mfumo wa kuthibitisha kuwasili kwa bidhaa kituoni (Proof of Delivery). Kupitia mifumo hii wateja wanaweza kuthibitisha kupokea mizigo kidijiti ambapo mfumo huu unafikika vituo zaidi ya 8700 nchi nzima. Mifumo hii imeongeza uwazi kwa kuwezesha vituo vya afya kutuma malalamiko moja kwa moja MSD, kufahamu taarifa zao za kifedha ikiwemo kufanya malipo, kufahamu hali ya mali ghalani, bei, hatua za oda kuanzia kupokelewa, kuchakatwa hadi kupokelewa na mteja kituoni, na pia taarifa hizi zinapatikana papo hapo (Real Time Tracking).
  4. Kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa magari kwa mfumo wa TEHAMA.
  5. Kuanza kufanya maboresho ya mfumo wa kizamani wa Enterprise Resource Planning (ERP) unaosimamia fedha, utunzaji, usambazaji na wateja kwenda kwenye mfumo wa kisasa unaojengwa mahususi kuendana na shughuli za Taasisi na mipango mikakati yake. Mradi huu unatarajia kurahisisha usimamizi, kufanya utendaji wa Bohari kuwa wa kisasa, wenye tija na huduma kwa wateja kuimarika.

5.4     Kuboresha Mnyororo wa Ugavi

Bohari ya Dawa ilikusudia kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya unaimarika, bidhaa za afya zinafika kwa wananchi kwa wakati na mabadiliko yanayotokea kwenye vituo vya kutolea huduma za afya yanafahamika MSD na hatua muhimu kuchukuliwa ili kuepusha ukosefu wa bidhaa za afya. Aidha, Bohari ya Dawa ilitambua umuhimu wa kujipanga na kuweza kukabiliana na majanga mbalimbali pindi yanapotokea na kuimarisha mifumo ili kuhakikisha bidhaa zinazopokelewa zinaendana na zile zilizoagizwa. Baadhi ya hatua na mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha mnyororo wa ugavi ni pamoja na;

  1. Kuwa na mpango maalum wa ununuzi unaolenga wazalishaji wa ndani pamoja na wale wa nje;
  2. Kufanikisha ununuzi wa bidhaa za huduma moja kutoka kwa mzabuni fanani ili kupunguza gharama za usimamizi na matengenezo, mfano; bidhaa zinazohusu uangalizi maalum kwa watoto kununuliwa kwa pamoja;
  3. Kufanya ugatuzi wa majukumu na kuwezesha Ofisi za Kanda kutekeleza majukumu mengi zaidi kwa kuhamisha baadhi ya shughuli zilizokuwa zikifanya Makao Makuu;
  4. Kuanza kutekeleza mpango wa ununuzi kwa kuzingatia mahali ambapo bidhaa zinapatikana kwa urahisi;
  5. Kuendelea kusimamia na kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa ndani ya MSD na zinazopokelewa kutoka kwa wazalishaji wengine zinakidhi ubora stahiki.

6.0     Utekelezaji wa Sera ya Viwanda.

Aidha, kwa kutambua jitihada za MSD, mwezi Oktoba 2021, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria ya MSD na kuongeza jukumu la uzalishaji na kuifanya MSD kuwa na majukumu makuu manne; Uzalishaji, Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vya umma vya kutolea huduma za afya.

Kutokana na umuhimu wa jukumu la uzalishaji na kwa kuhakikisha MSD inatekeleza majukumu yake kiufanisi, mnamo tarehe 18 Aprili 2023, anzisha Kampuni Tanzu ijulikanayo kama MSD Medipharm Manufacturing Company Limited yenye namba za usajili 165103548. Kampuni imekasimiwa jukumu la uzalishaji ili kuongeza ufanisi na tija katika kukuza viwanda vya uzalishaji wa bidhaa za afya nchini.

Ili kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi, kampuni tanzu ya Medipharm inafanya shughuli za uwekezaji wa viwanda vya bidhaa za afya kwa utaratibu mbalimbali ikiwemo ubia (Joint Venture) na wawekezaji binafsi ili kupata teknolojia, kukuza mtaji na kuongeza kasi ya ukuaji wa viwanda. Kwa sasa viwanda vyote vinavyomilikiwa na MSD pamoja na miradi ya uwekezaji katika uzalishaji bidhaa za Afya vipo chini ya kampuni hii. Kampuni hii ina Bodi yake ambayo ina wajumbe watano (5). Baadhi ya viwanda vinavyosimamiwa na Kampuni Tanzu ni pamoja na;

6.1      Kiwanda cha uzalishaji wa Barakoa.

Kiwanda hiki kilichopo Keko, Dar es salaam kilianza mwaka 2020 na kina uwezo wa kuzalisha wastani wa barakoa 6,000,000 kwa mwaka na uwekezaji wake uligharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.37. Kiasi hichi kinajumuisha gharama za uwekezaji na uendeshaji kwa mwaka wa kwanza. Aidha, mwezi Machi 2023 MSD ilipata msaada ya mitambo ya kuzalisha barakoa za N95 yenye thamani ya Euro 89,192.3 (sawa na shilingi milioni 224.9) kutoka Serikali ya Japan kupitia UNIDO na kuongeza uwezo wa Kiwanda na kufikia barakoa milioni 10.8 kwa mwaka. Kufikia tarehe 30 Juni 2025, kiwanda cha barakoa kilizalisha na kuuza jumla ya barakoa 9,280,206 zenye thamani ya shilingi bilioni 5.2 ambazo ziliuzwa kwa vituo mbalimbali nchini na hivyo tayari kimeweza kurudisha fedha yote ya uwekezaji. Aidha, uzalishaji wa bidhaa hizi umefanya nchi iache kabisha kununua bidhaa hizi kutoka nje ya nchi.

6.2     Kiwanda cha uzalishaji wa Mipira ya Mikono 

Kiwanda hiki kilianza ujenzi wake mwaka 2021 na kimekamilika mwaka 2024 ambapo kilianza rasmi uzalishaji wa Mipira ya Mikono ya Uchunguzi (Examination Gloves). Aidha, kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha hadi vipande vya Mipira ya Mikono milioni 48.8 kwa mwaka na uwekezaji wake umegharimu jumla ya shilingi bilioni 25 ikijumuisha ununuzi wa mitambo, ujenzi wa majengo na malighafi ya uzalishaji kwa mwaka wa kwanza. Kufikia mwezi Juni 2025, Kiwanda kimezalisha na kuuza jumla ya vipande vya mipira ya Mikono milioni 5.6 zenye thamani ya shilingi bilioni 1.2.

Uwepo wa kiwanda hiki umetengeneza zaidi ya ajira 100 na kuweza kupunguza utegemezi wa bidhaa hizi kutoka nje.

6.3     Miradi ya Ubia ya Uzalishaji wa bidhaa za afya

Kwa sasa Kampuni tanzu “MSD Medipharm Manufacturing company Limited” imeingia makubaliano ya uwekezaji wa pamoja (Joint Venture) na Kampuni ya Rotabiogen East Africa inayomilikiwa na Rotabiogen ya nchini Misri na matarajio ni kujenga kiwanda cha kuzalisha dawa za maji za Sindano katika eneo Maalum la Viwanda na Uchumi la MSD (MSD Special Industrial Economic Zone) la Zegereni, Kibaha Mkoa wa Pwani. Aidha, majadiliano ya fursa za ubia yanaendelea na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi walioonesha nia ya kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa za afya nchini ikiwemo Uzalishaji wa bidhaa za afya za Pamba Mkoani Simiyu, Mipira ya Kiume (Condoms), na dawa za maradhi sugu ya Saratani na nyingine kwa kushirikiana na Bohari ya Dawa kupitia kampuni tanzu yake ya MSD Medipharm.

Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia nchi kupunguza uagizaji wa dawa muhimu za sindano kutoka nje ya nchi na kuongeza upatikanaji wa bidhaa na kuimarisha utoaji huduma za afya katika vituo vya afya nchini.

 7.0    Ujenzi wa Maghala ya Kuhifadhi Bidhaa za Afya

Katika kipindi cha kati ya mwaka 2012 hadi 2022, idadi ya watu imeongezeka kutoka watu milioni 43.5 na kufikia milioni 59.9, sawa na asilimia 38, kwa kanda zinazo hudumiwa na MSD. Kutokana na ukuaji wa mahitaji, idadi na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali, Bohari ya Dawa ilifanya tathmini ya kuwezesha kutambua uhitaji wa miundombinu ya utunzaji wa bidhaa za afya ambayo imeonesha MSD inamiliki mita za mraba 36,254 sawa na asilimia 36 ya mahitaji halisi ya kutosheleza utunzaji wa bidhaa za afya ni mita za mraba 100,000.

Kwa kutambua upungufu huo, Bohari ya Dawa ilianza mradi wa ujenzi wa maghala ambao uligawanywa kwa Awamu III;

  1. Awamu ya I ikiwa ni ujenzi wa Ghala kwenye mikoa ya Dodoma na Mtwara
  2. Awamu ya II ni ujenzi wa Ghala katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Geita
  3. Awamu ya III ni ujenzi wa Ghala kwenye mikoa ya Ruvuma na Iringa

7.1 Awamu ya I: Ujenzi wa Ghala la Dodoma na Mtwara

Hadi kufikia mwezi Juni 2025, ujenzi wa maghala ya Mtwara na Dodoma ulikuwa umekamilika. Ujenzi wa maghala haya yenye jumla ya mita za mraba 12,000 umegharimu shilingi bilioni 42 na yanatarajia kukidhi uhitaji wa kuwezesha uhifadhi bora wa bidhaa za afya na kupunguza gharama za uendeshaji.

Picha 2: Ghala la jipya lililopo mkoa wa Mtwara

Ghala la Dodoma lina ukubwa wa mita za mraba 7,200 na limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 23.7. Ghala hili litakuwa kiungo cha maghala yaliyopo kwenye kanda 5: Mwanza, Kagera, Tabora, Iringa na Dodoma na hivyo kuwezesha usafirishaji wa haraka kwa kutumia miundombinu ya treni ya kisasa (SGR), hivyo kupunguza gharama za kufuata bidhaa Dar es Salaam ambapo bidhaa nyingi huingilia bandarini. Ghala hili litasaidia uhifadhi wa bidhaa za afya kwenye viwango stahiki na kuwezesha nchi kuwa na usalama wa bidhaa za afya hasa kipindi cha majanga na milipuko kwa kuwa ghala hili litakuwa ni kitovu cha uhifadhi cha katikati ya nchi (Central Hub). Aidha, ghala hili litawezesha bidhaa kupatikana kwa wananchi kwa karibu.

Ghala la Mtwara litakuwa mbadala wa ghala chakavu na finyu lililokuwepo, lisilo na viwango na ambalo lilikuwa likihatarisha usalama na ubora ya bidhaa za afya, na watumishi kutokana na kuwa karibu na bandari ambapo vumbi la makaa ya mawe limekuwa likitokea. Aidha, ghala hili litatoa uhakika wa bidhaa za afya kupatikana kutokana na ghala la awali kuwa finyu hivyo kulazimika kusafiri mara kwa mara kufuata bidhaa zinapoisha na kushindwa kuhudumia vituo vya kutolea huduma za afya kwa wakati.

7.2 Awamu ya II: Ujenzi wa Ghala katika mikoa ya Dar es Salaam, Geita na Mwanza

Bohari ya Dawa inatarajia kukabidhi rasmi kwa mkandarasi eneo la ujenzi wa ghala la Chato mkoani Geita mnamo tarehe 20 Agosti 2025. Ghala hili litakuwa na ukubwa wa mita za mraba 4,800 na litahudumia vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo mkoa wa Kagera, Geita na baadhi ya Halmashauri za Mkoa wa Kigoma. 

Vilevile, Bohari ya Dawa inatarajia kupokea kiasi cha shilingi bilioni 13 kuwezesha kuanza kwa ujenzi wa Ghala la Mwanza. Hadi sasa, Bohari ya Dawa imeweza kuandaa mchoro ambao utatumika kwenye ujenzi wa ghala hilo na ukamilishaji wa hatua nyinginezo za maandalizi unaendelea.

Aidha, Bohari ya Dawa inatarajia kuanza ujenzi wa ghala la Dar es Salaam ambapo Serikali imefanikiwa kuwezesha kupatikana kwa fedha hizo kupitia vyanzo vyake. 

8.0     Utekelezaji wa mradi wa matumizi ya Nishati Mbadala 

Bohari ya Dawa imekuwa ikikabiliwa na gharama kubwa ya nishati ya umeme ya kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kwa mwaka kutokana na utunzaji unaohitajika wa bidhaa za afya. Hivyo kuhitaji matumizi ya nishati mbadala kuhakikisha taasisi inatekeleza majukumu yake ya utunzaji kwa ufanisi. Kutokana na mipango ya ujenzi wa maghala unaoendelea, gharama ya nishati ya umeme itaongezeka hivyo kuhitajika nishati mbadala ili kuweza kupunguza gharama hizi na kuongeza ufanisi. 

Matarajio ya usimikaji wa nishati mbadala itokanayo na umeme wa jua ni kuweza kupata faida kutokana na malipo ya hewa ya ukaa “carbon credit”, uokoaji wa fedha za matumizi ya nishati na kuendana na mahitaji ya viwango vya utunzaji wa bidhaa za afya. Matarajio ya mradi ni kuweza kuishi kwa muda wa miaka 25 na fedha zitakazowekezwa zitakuwa zimerudi ndani ya miaka 11. Gharama za utekelezaji wa huu mradi ni kiasi cha Dola za Kimarekani 13,971,300 sawa na shilingi bilioni 38.1. Uwepo wa nishati hii itasaidia kuendana na mpango mzima wa Serikali wa kuhimiza matumizi ya nishati mbadala na utunzaji wa mazingira, utasaidia kuimarisha uhifadhi wa bidhaa za afya na kuokoa fedha nyingi zinazotumika katika shughuli za kila siku za Bohari ya Dawa. 

Hadi sasa, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 4.6 ili kutekeleza mradi wa umeme wa jua kwenye maghala yaliyopo Dodoma na Mtwara.

9.0     Mpango wa Uanzishaji wa Kampuni Tanzu ya Usambazaji

Katika kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini, Bohari ya Dawa imeweka mkakati wa ugatuzi wa jukumu la usambazaji wa bidhaa za afya kwenda kwa Kampuni Tanzu. Lengo kuu la ugatuzi huu ni kuongeza ufanisi, kupunguza urasimu katika maamuzi, kuongeza tija katika matumizi ya rasilimali mbalimbali za usambazaji, kukuza teknologia, pamoja na kutafuta fursa za kibiashara nje ya huduma zitolewazo na MSD. Mkakati huu wa ugatuzi utapunguza matumizi na vilevile kuongeza mapato kwa kutanua wigo wa biashara ya usambazaji.

Kampuni tanzu hii imepata idhini ya Bodi ya Wadhamini mwezi Februari 2025 na inatarajiwa kuwasilishwa kwa Wizara ya Fedha na kisha Msajili wa Hazina kwa ajili ya ridhaa ya kusajiliwa rasmi. Hatua hii ni matokeo chanya ya msukumo wa kimageuzi wa awamu ya sita unaolenga kuongeza tija na ufanisi kwa Bohari ya Dawa ili iweze kujiendesha kibiashara na kufikisha huduma kwa wananchi kwa wakati na kwa bei nafuu.

10.0   Ununuzi wa Pamoja kupitia - Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika (SADC)

Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2024/25, Bohari ya Dawa imepiga hatua katika kutekeleza mpango wa ununuzi wa pamoja wa bidhaa za afya katika nchi wanachama wa SADC (SADC Pooled Procurement Services, SPPS).

Mwaka 2021/2022, Bohari ya Dawa (MSD) ilifanya manunuzi ya dawa kwa nchi tatu (Comoros, Seychelles, Tanzania), na kuokoa kati ya 50-70% ya gharama. Hii iliwezekana kutokana na Bohari ya Dawa kuunda muongozo wa ununuzi wa pamoja nchi wanachama, kuandaa orodha ya bidhaa za afya ambayo nchi wanachama wa SADC waliridhia itumike kwenye ununuzi wa pamoja, na kuingia mikataba na washitiri iliyopelekea ununuzi wa pamoja.

Kutokana na changamoto za utekelezaji wa ununuzi wa pamoja, Serikali imejikita kwenye kufanya maboresho yenye lengo la kuhakikisha ununuzi wa pamoja unafanikiwa.  Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na;

  1. Bohari ya Dawa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali mtandao (eGA) kuunda mfumo wa kielektroniki (e-SPPS), ambao utatumika na nchi wanachama kwenye kuweka oda zao za bidhaa za afya wanazohitaji, na kuweza kufuatilia hatua mbalimbali ya manunuzi.
  2. Kufanikisha kuandaa, kuwasilisha na kupitishwa kwa rasimu ya mpango wa biashara wa SPPS na kikao cha baraza la mawaziri Machi 2025. Mpango huu wa biashara wa SPPS unatoa mwongozo wa jinsi nchi wanachama SADC watakavyoweza kushiriki kwenye ununuzi wa pamoja.
  3. Kufanya uhamasishaji wa kutumia huduma ya ununuzi wa pamoja wa SPPS ulifanyika kwa nchi saba za SADC - Namibia, Eswatini, Botswana, Zambia, Zimbabwe, Malawi na Congo. Juhudi za uhamasishaji zinalenga kuongeza uelewa na kukuza ushiriki wa nchi hizi katika mfumo wa SPPS.

11.0   MWELEKEO WA BOHARI YA DAWA KWA MWAKA 2025/2026

Katika kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Bohari ya Dawa, Vipaumbele Vifuatavyo vimewekwa kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.

  1. Kupitia Kampuni Tanzu, Bohari ya Dawa itaendelea na jitihada za kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza idadi ya viwanda vya bidhaa za afya nchini hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni. Aidha, Bohari ya Dawa inaendelea kutumia Kituo cha Uwekezaji na balozi zetu ili kuweza kuvutia wawekezaji wenye lengo la kufanya uzalishaji nchini. Jitihada hizi zinafanyika kwenye uwekezaji kwenye bidhaa za ARV (dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI), mipira ya kiume (Condoms), bidhaa za afya zitokanazo na pamba, dawa mchanganyiko na bidhaa nyinginezo. Jitihada hizi ni pamoja na kushiriki kikamilifu katika kufufua na kuendeleza Kiwanda cha Dawa cha Keko na cha Arusha.
  2. Kuongeza Uwezo wa Usambazaji na Uhifadhi wa Bidhaa za afya

Kutokana na ongezeko la mahitaji na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya, Bohari ya Dawa itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya maghala na magari yenye ufanisi ili kuongeza ufanisi kwa kuweza kufikisha bidhaa kwa wakati, ubora na gharama. 

  1. Uwekezaji katika Nishati Mbadala

Katika kuhakikisha Bohari ya Dawa inaendana na malengo ya uendelevu, shughuli zake za utendaji zitazingatia uwekezaji wenye lengo la kupunguza kiwango cha uzalishaji wa kaboni, kuongeza ufanisi wa nishati, na kuimarisha mnyororo wa ugavi.

  1. Mageuzi ya TEHAMA

Bohari ya Dawa imedhamiria kuendelea kuboresha ufanisi wa uendeshaji na utoaji wa huduma kwa kutumia TEHAMA. Bohari ya Dawa imeweka kipaumbele katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali na ubunifu ili kurahisisha kazi na kuendana na mabadiliko yanayotokea Ulimwenguni.

  1. Kuendelea kushiriki katika kukuza uzalishaji wa bidhaa za afya nchini

Bohari ya Dawa itaendelea kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha viwanda vya ndani vinapata fursa ya soko lililopo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Hali itafanikiwa kwa kuandaa zabuni maalumu kwa wazalishaji wa ndani na kutoa vipaumbele kwa mujibu wa Sheria.

Aidha, Bohari ya Dawa kupitia Kampuni yake Tanzu, MSD Medipharm Manufacturing Company Limited, itaendelea kufanya jitihada za kuvutia wawekezaji kwa njia ya ushirikiano ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa za afya nchini. 

  1. Kuboresha Utoaji wa Huduma

MSD itaboresha utendaji wa mnyororo wa ugavi kwa kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya, kutimiza mahitaji ya wateja, kuimarisha hatua za uhakiki wa ubora, na kukuza mahusiano na wateja wa kibiashara ili kujenga ushirikiano wa manufaa kwa pande zote. Hii itahusisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama TMCHIP, MCHIP, Dialysis, CEmONC, GFATM, dawa za saratani, magonjwa ya afya ya akili, magonjwa ya moyo, na mengineyo. Zaidi ya hayo, MSD itaimarisha utoaji wa huduma kwa wateja wa kibiashara ili kusaidia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

Ajouter un commentaire

HTML restreint

  • Vous pouvez aligner les images (data-align="center"), mais également les vidéos, citations, etc.
  • Vous pouvez légender les images (data-align="center"), mais également les vidéos, citations, etc.

About

MSD a été créée pour produire, acheter, stocker et distribuer les produits de santé approuvés nécessaires aux établissements de santé. Dans le cadre de cette mission, nous veillons à ce que les produits de santé en Tanzanie soient accessibles, fiables et abordables, et livrés à temps dans tous les établissements de santé en Tanzanie et au-delà.

Featured Posts

Contact info

Notre mission : Rendre les produits de santé de qualité accessibles à tous les établissements de santé publics en Tanzanie.